Ukiona watu wengine walivyo na ujasiri wa kuyaishi maisha yao, unaweza kufikiri ni wewe peke yako ambaye hofu zimekutawala.

Ukiona wengine wakiwa na hamasa ya kufanya makubwa kwenye maisha yao, unaweza kufikiri ni wewe peke yako ambaye huna hamasa ya kuchukua hatua.

Ukiona wengine wakiwa na maisha tulivu yasiyo na changamoto nyingi, unaweza kufikiri ni wewe pekee ambaye maisha yako yamejaa kila aina ya changamoto.

Lakini leo nataka nikuhakikishie kitu kimoja, siyo wewe peke yako.

Kila unayemuona anapambana na mambo unayopambana nayo wewe, hofu, kukosa hamasa, changamoto, uchovu na mengine mengi.

Wale unaowaona wanapiga hatua licha ya kuwa na mambo hayo siyo kwa sababu hayapo kwao, ila kwa sababu wamechagua kupiga hatua licha ya kuzungukwa na mambo hayo.

Ungeona yale ambayo wengine wanapambana nayo, ungeshangaa jinsi ambavyo mambo yako ni madogo. Utashangaa jinsi ambavyo wengine wanapambana na makubwa lakini hawakatishwi tamaa, wanazidi kupiga hatua.

Hivyo pambana na hali yako, usifikiri ni wewe pekee unapitia hilo, jua kila mtu anapigana vita yake, pigana yako pia, usikate tamaa.

Kwa chochote unachopitia, kazana kusonga mbele. Angalia ni nini unachoweza kufanya kwa pale ulipo, badala ya kuangalia kipi kinachokukwamisha. Kama ambavyo Martin Luther King Jr alivyowahi kusema, kama huwezi kupaa basi kimbia, kama huwezi kukimbia basi tembea na kama huwezi kutembea basi tambaa, kwa chochote unachofanya, hakikisha unasonga mbele, hubaki pale ulipo sasa.

Songa mbele, usikubali kubaki pale ulipo, usiruhusu chochote kiwe kikwazo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha