“Service to others is the rent you pay for your room here on earth.” – Muhammad Ali

Dunia siyo makazi yetu ya kudumu, ni sehemu ambayo tumepanga kwa muda tu.
Kama tunavyojua, kila unapokuwa umepanga eneo unapaswa kulipa kodi ya pango.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa maisha yetu hapa duniani, tunapaswa kulipa kodi ya pango.

Kodi ya pango tunaloishi hapa duniani ni huduma tunayotoa kwa wengine.
Kuwahudumia wengine ndiyo wajibu wetu mkuu, ndiyo kinachokamilisha ubinadamu wetu.
Kutambua hili na kulifanya vyema kunasaidia maisha yetu kuwa bora.

Kwa kila unachofanya, swali kuu unalopaswa kujiuliza ni kwa namna gani unawahudumia wengine.
Usijiangalie tu wewe unapata nini, bali angalia wengine nao wananufaikaje.
Zipo njia nyingi za kuwahudumia wengine na kila aina ya kazi au biashara tunazofanya, ni sehemu ya huduma kwa wengine.
Wajibu wetu ni kufanya kile tunachofanya kwa mtazamo sahihi, mtazamo wa kuangalia wengine wananufaikaje.

Kuwahudumia wengine hakuyakamilishi tu maisha yao na yetu, bali pia kunawavutia wengi zaidi kuja kwetu.
Ukiwahudumia watu vizuri, matokeo yataonekana na wengi na hao pia watakuja kwako wakitaka uwahudumie.
Hutahitaji kupiga kelele sana kuwapata watu, bali huduma unayotoa itakusemea.

Kuwa mtu wa huduma, kwa kila unachofanya, msisitizo wako unapaswa kuwa jinsi unavyowahudumia wengine.
Kwa kufanya hivyo utakuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kufyeka au kung’oa, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/12/01/2162

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.