Ipo kauli ya Kiswahili inayosema wema huzaa dhambi.

Ni kauli ya kutahadharisha kwenye wema ambao mtu anakuwa nao kwa sababu kuna wakati unampofusha na hatimaye kuleta matatizo makubwa.

Upofu wa wema uko kwenye mtu kudhani wengine nao ni wema kama wao.

Mara nyingi watu ambao ni waaminifu ndiyo huwa wanaishia kulaghaiwa na watu wasio waaminifu.

Hiyo ni kwa sababu uaminifu wao huwafanya waone kila mtu ni mwaminifu kama wao.

Walio wa kweli ndiyo huwa rahisi zaidi kudanganywa na wasio wa kweli, hiyo ni kwa sababu kwa kuwa ni wa kweli, wanaamini kila mtu ni mkweli kama wao.

Hata kwenye kazi, wachapakazi huwa wanalaghaiwa na wasio wachapa kazi, hasa kwenye kuweka ahadi fulani. Ni kwa sababu wanafikiri kila mtu ni kama wao.

Kwa upande wa pili, wasio wema, wasio waaminifu na wasio wa kweli, huwa wanaweza kuepuka wasiumizwe na wengine kwenye hayo kwa sababu wanachukulia kila mtu ni kama wao.

Kwa kutambua hili, tunapaswa kuwa makini kwa wale tunaoshirikiana nao, siyo kwa kuwachukulia kama wasio sahihi, ila kuepuka kuwahukumu kwa kujitumia wewe.

Kwa mtu yeyote yule, kama hujamjua kwa tabia zake za ndani, usijiaminishe chochote kuhusu yeye. Mchukulie kama usiyemfahamu na jifunze kupitia matendo yake na siyo maneno yake.

Mpe kila mtu nafasi ya kufanya vizuri au kukosea, na siyo kuwahukumu kwa jinsi wewe ulivyo.

Na penda kuwapima watu kwa matendo yao, hasa yale wanayoyafanya wakati hakuna anayeangalia. Hayo ndiyo yatamuelezea mtu kwa ukweli kuliko anachosema au anachofanya akiwa anaonekana na wengine.

Na pale unapohitaji kufanya maamuzi ya haraka kuhusu mtu, huku ukiwa huna muda wa kumchunguza na kumjua, basi chukulia ni mtu aliye kinyume kabisa na tabia zako hivyo kuchukua tahadhari kuhakikisha hudhuriki na maamuzi unayokwenda kufanya.

Kwa kujua na kufanya hivyo, unajiweka kwenye nafasi ya kutokuumiza au kuangushwa na yale ambayo wengine wanafanya au kutokufanya. Hutamlalamikia yeyote kwa sababu unajua siyo kila mtu yuko kama wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha