Kama huipendi kazi au biashara unayofanya, kama unachofanya kinakupa msongo na huna hamasa ya kufanya kwa ukubwa zaidi, tatizo linaweza kuwa huzalishi matokeo ya kutosha au huoni athari ya matokeo unayozalisha.

Ukitatua hayo mawili, kwa kuanza na unachozalisha na kisha ukafuatilia athari za unachozalisha, utapenda kile unachofanya na kuhamasika kufanya zaidi.

Zig Zigler kwenye moja ya mafundisho yake ya hamasa amewahi kutoa mfano wa mabinti wawili ambao walikuwa wahudumu kwenye mgahawa. Walikuwa hawaipendi kazi hiyo na waliifanya basi tu. Siku moja waliamua waachane na kazi hiyo na kwenda kufanya mambo mengine.

Wakakubaliana wachague siku ya mwisho kwenye kazi hiyo, siku ambayo wataifanya kazi kwa moyo wao wote halafu siku inapoisha wamfuate meneja na kumweleza hawaendelei tena na kazi.

Wakaichagua siku na wakaianza kwa hamasa kubwa, wakahudumia wateja kwa moyo wote na cha kushangaza wateja wakawa wanawashukuru na kuwaachia chenchi kama zawadi (tip). Mpaka wanafika mwisho wa siku hiyo, walikuwa wamepata shukrani nyingi kutoka kwa wateja na kiasi kikubwa cha zawadi ya fedha.

Ulipofika muda wa kumaliza kazi, binti mmoja alimuuliza mwenzake, tunaenda saa ngapi kwa meneja kumweleza mpango wetu wa kuacha kazi? Mwenzake akamjibu hana tena mpango wa kuacha kazi, bali atakuwa anaifanya kila siku kama alivyoifanya siku hiyo ya mwisho.

Mfano huu una somo kubwa, unaweza kuona kazi au biashara unayofanya haifai, huipendi au hailipi kumbe tatizo ni namna unavyoifanya, huzalishi matokeo mazuri au huoni athari za matokeo ya unachozalisha.

Ndiyo maana nimekuwa nashauri chochote unachofanya, hakikisha kuna namna mwingine ananufaika, jua ni tatizo au hitaji gani la wengine unalotatua kupitia unachofanya. Kwa kufanya hivyo, utapenda unachofanya na kukifurahia.

Na kama unafanya hivyo ila bado hupendi au hupati hamasa ya kuendelea kufanya, basi omba ushuhuda kwa wale wanaonufaika na unachofanya. Waombe wakuambie ni jinsi gani kazi au biashara yako imebadili maisha yao. Utasikia hadithi nzuri na zitakupa hamasa ya kuendelea kufanya zaidi.

Kabla hujasema unachofanya hukipendi au hakilipi, hakikisha kwanza unazalisha matokeo mazuri na unajua athari za matokeo hayo kwa wale wanaoyapokea. Kwa sababu kama utakimbilia kwenye kitu kingine bila ya kutatua changamoto ya uzalishaji wako, huko nako hutakaa muda mrefu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha