Moja ya sababu zinazopelekea mahusiano ya mbali yasidumu, ni urahisi wa maneno kuchukuliwa tofauti na aliyeyasema alivyomaanisha.
Moja ya sababu ya watu kutokuelewana na kutukanana mitandaoni, ni urahisi wa alichoandika mtu kuchukuliwa kwa namna tofauti na alivyomaanisha.
Watu mnapokuwa ana kwa ana mazungumzo huwa yanaendana na muktadha. Kama mpo kwenye hali ya furaha au huzuni, mazungumzo yataendana na muktadha huo. Na kila mtu ataelewa kwa sababu yuko kwenye eneo hilo.
Lakini inapokuwa ni mawasiliano ya walio mbali, muktadha unapotea, kwa sababu kila mtu yuko kwenye hali tofauti. Hivyo anayetuma ujumbe anaweza kuwa na nia njema, ila anayeupokea akautafsiri vibaya na hapo ndipo hali ya kutokuelewana inapoanzia.
Kwa kujua hili, tunapaswa kuwa makini sana na mawasiliano yetu, hasa yale ya mbali. Unapofanya mawasiliano hayo, usiangalie muktadha wako tu, angalia na wa yule unayewasiliana naye.
Kwa kuwa huwezi kujua mtu atakuwa kwenye hali gani wakati anapokea mawasiliano yako, ni bora kuwa makini na mawasiliano unayotuma, kuhakikisha kwa muktadha wowote mtu anaokuwa nao, hatayatafsiri vibaya.
Tungekuwa tunazingatia hili, tungeepusha changamoto nyingi tunazoanzisha kutokana na mawasiliano ya mbali. Mara zote zingatia kwamba watu wanaweza kutafsiri tofauti na ulivyomaanisha, hivyo boresha mawasiliano yako kwa namna ambayo hayatatafsiriwa tofauti.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha, ni ukweli mtupu huu. Ubarikiwe kwa makala.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike