Kazi yako siyo kutetea kile unachokifanya,
Kazi yako siyo kumridhisha na kumfurahisha kila mtu,
Kazi yako siyo kutaka uonekane kwa unachofanya,
Bali kazi yako ni kufanya kazi yako, kwa namna ambayo inaongeza thamani kubwa kwa wengine na kukuingizia wewe kipato cha kuendesha maisha yako kwa namna inayokuweka huru.
Inashangaza jinsi ambavyo watu wanapoteza muda na nguvu kwenye mambo mengine yasiyo kazi zao, mambo ambayo hayana msaada kwa yeyote yule.
Kujifunza kuhusu kazi yako ni kazi yako, kukazana kuwa bora kwenye kazi yako ni kazi yako, hayo ni sehemu ya kazi.
Lakini mengine, kupambana na wale wanaokukosoa kwa kazi yako siyo matumizi mazuri ya rasilimali zilizo muhimu kwako. Unaweza kusikiliza ukosoaji wao na kama kuna mahali hapajawa sahihi unaweza kuparekebisha lakini usipoteze rasilimali muhimu nje ya kazi yako.
Ifanye kazi yako na hiyo ndiyo itakayokuweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa na maisha unayoyataka, mengine yote ambayo hayana mchango kwenye kazi yako, achana nayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,