Akili yako inahitaji kupata mapumziko, hasa baada ya kufanya kazi nzito za kujifunza, kufikiri na kufanya maamuzi.
Lakini haitapata mapumziko hayo kwa kutumia vilevi, hivyo huchosha zaidi mwili na akili.
Pia akili haitapata mapumziko kwa kuangalia tv au kuperuzi mitandao ya kijamii, huko utaisisimua zaidi akili na kuichosha.
Kadhalika akili haitapata mapumziko kwa kutazama michezo mbalimbali au kushiriki mijadala na mabishano, yote hayo yanaichosha zaidi akili.
Katika kuipumzisha akili unapaswa kuchagua vitu ambavyo havikuhitaji ufikirie sana na pia havichochei hisia zako.
Unaweza kuipumzisha akili kwa kufanya tahajudi, hapo unalenga fikra zako kwenye kitu fulani kinachojirudia rudia na hivyo huhitaji kutumia nguvu kubwa.
Unaweza kuipumzisha akili kwa kutembea kwenye asili, zoezi ambalo litaifanya akili ione mambo mazuri na kuwa na utulivu.
Pia unaweza kuituliza akili kwa kufanya kile unachopenda kufanya (hobby) ambacho hakuna anayetegemea uzalishe matokeo fulani au anakulipa kufanya.
Aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Uingereza, Winston Churchill amewahi kusema kila mtu anahitaji kuwa na hobi, ambayo itakuwa sehemu yake ya kuipumzisha akili baada ya kazi nzito.
Yeye mwenyewe alikuwa na hobi mbili, kuchora na kujenga matofali. Katika kipindi cha maisha yake alifanya michoro mingi, ambayo ilikuwa ya kawaida kabisa kwa sababu hakuifanya kama sehemu ya sanaa, bali aliifanya kama sehemu ya kupumzisha akili. Pia kuna wakati alikaa nje ya mji na kufanya kazi za mikono kama kujenga matofali, kukata magogo na kadhalika.
Changamoto kubwa ya zama hizi ni watu wengi hawana hobi na hilo limetokana na mitandao ya kijamii kumeza muda wa kila mtu, kwa sasa kila muda usio na kazi ambao mtu anaupata, anaumalizia kwenye mitandao, michezo au mambo mengine yasiyopumzisha akili.
Lakini pia kwa wale ambao wameweza kufanyia kazi hobi zao, zimebadilika na kuwa kazi au biashara. Walianza kwa kupenda kufanya, baadaye watu wakawataka wawafanyie na watawalipa, baadaye hobi zikageuka kuwa njia ya kuingiza kipato na hapo zikaacha kuwa hobi. Mtu anakuwa hana tena kitu cha kumpumzisha.
Hata kama hobi yako ya zamani umeshaigeuza kuwa njia ya kuingiza kipato, chagua hobi nyingine ambayo utaifanya kwa ajili yako, ili iwe sehemu ya kuipumzisha akili yako.
Kuna uhuru mkubwa pale unapofanya kitu kwa sababu umechagua kufanya, ukijua hakuna anayekuangalia au kukuhukumu kwa namna unavyofanya. Hapo ndipo akili inakuwa huru, inapumzika na hata ubunifu unaibuka.
Kuwa na utaratibu wa kupumzisha akili yako kwa kufanya tahajudi, kutembea kwenye asili na kuwa na hobi unayoifanya kwa ajili yako tu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,