Jamii ikitaka kututega tufanye kitu, huwa inakiweka kwa namna ya mashindano.
Kukishakuwa na hali ya kushindana, hata kama ushindi hauna zawadi, mtu utasukumwa kushindana ili ushinde.
Unafikiri nini kinafanya mitandao ya kijamii ipate watumiaji wengi na wanaoitumia kwa muda mrefu?
Ni hali ya mashindano, pale mmoja anapoona mwenzake ana wafuasi wengi, na yeye anakazana apate wafuasi wengi pia, hata kama kuwa na wafuasi wengi hakumuongezei chochote.
Kadhalika michezo ya kielektroniki (Games) huwa inaweka hali ya mashindano na hiyo huwafanya watu wawe na uraibu nayo na kuicheza kwa muda mrefu.
Akili zetu zinapenda mashindano kwa sababu kila unaposhinda ubongo unaachilia kemikali ya dopamini inayokufanya ujisikie vizuri. Na hivyo watu wanaokutaka ufanye kitu fulani, wanakiweka kwa namna itakayoleta ushindani ili unase kwenye kukifanya.
Kwa kujua hili, kuwa makini na kila aina ya ushindani unayoshawishiwa kuingia, kwa kila unachofanya, kikague, je umepanga mwenyewe kufanya na kuna manufaa au umejikuta tu unafanya kwa sababu umeona wengine pia wanafanya?
Huwa kuna kichekesho kwamba mtu alikuwa anafanya mazoezi ya kukimbia barabarani, mara ghafla mkimbiaji mwingine akampite, akajikuta anakaza mwendo ili ampite, mwishowe akajikuta amefika sehemu ambayo hakukusudia.
Kinaonekana ni kichekesho, lakini kimebeba ujumbe mkubwa na kwa sehemu kubwa hivyo ndivyo wengi wanavyoendesha maisha yao. Wanajikuta wametingwa kweli kweli katika kufanya kitu, lakini hakuna manufaa yoyote kwake.
Ni muhimu sana kila unapoianza siku yako kujiwekea vipaumbele vyako kwenye siku hiyo, kabla hata hujasumbuliwa na chochote na fuata mpango wako kwenye siku yako.
Usipokuwa na vipaumbele ulivyoanza navyo mwenyewe, watu hawatakuacha salama, watakunasa kwenye mashindano utakayopambana kwa juhudi kubwa, lakini yasiyo na manufaa yoyote kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,