Utajiri wa zamani ulijengwa kwenye misingi ya uhaba, kwamba rasilimali muhimu ni chache, wachache wanazihodhi na kunufaika kwa kiwango kikubwa.

Hivyo ndivyo zama za kilimo zilivyofanya kazi, wachache walimiliki mashamba na wengi kuwa wafanyakazi au watumwa kwenye mashamba hayo.

Kadhalika zama za viwanda zikarithi hilo, kumiliki kiwanda ilihitaji mtaji mkubwa, wachache waliopata mtaji huo walizuia wengine wasiingie na kutengeneza ushindani.

Mfumo huo wa utajiri ulifanya kazi kwamba kadiri kitu kinavyokuwa na uhaba, ndivyo wengi wanakuwa tayari kulipa zaidi ili kukipata. Hivyo kama kuna kiwanda kimoja pekee kinachozalisha bidhaa fulani muhimu, kila mtu atakuwa tayari kuinunua kwa bei ambayo kiwanda kimepanga.

Kuhodhi soko ndiyo ilikuwa tatizo kubwa la mfumo wa ubepari, kwamba wachache wenye nguvu wanalikamata soko na kutumia nguvu yao kujinufaisha zaidi.

Sasa tunaishi kwenye zama za taarifa, ambapo uhaba umefutika kabisa. Angalia jinsi kulivyo na mafuriko ya maarifa na taarifa za kila aina, kwa simu yako ya mkononi tu, unaweza kupata taarifa na maarifa mengi kuliko aliyokuwa anayapata raisi wa marekani wakati wa vita ya pili ya dunia.

Uchumi wa zama hizi umejengwa zaidi kwenye koneksheni badala ya kuhodhi, wale wenye koneksheni ambazo ni nzuri, ndiyo wanaotajirika zaidi. Hivyo badala ya kujenga utajiri wako kwenye uhaba, unapaswa kuujenga kwenye thamani.

Unapaswa kuzalisha thamani kubwa kwa wale unaowalenga, thamani bora na ya kipekee na yenye manufaa makubwa kwao, kwa namna ambayo wewe tu ndiye unayeweza kufanya.

Kwa kuchagua njia hiyo huhitaji kushindana na yeyote, wala huhitaji kumzuia mwingine asipande, nguvu zako zote unazipeleka kwenye kuzalisha thamani kwa wale unaowalenga.

Katika zama hizi hakuna tena soko moja kubwa, bali kuna masoko madogo madogo mengi.

Katika zama hizi huhitaji kujiuliza utatengenezaje fedha, badala yake unapaswa kujiuliza unatengenezaje koneksheni zitakazokuletea fedha zaidi. Lazima uwachague watu ambao tayari wana fedha na wewe una kitu wanachohitaji sana, unawapa kitu hicho na wao wanakupa fedha.

Huhitaji kuomba wala kuonewa huruma ndiyo upate fedha hizo, unachohitaji ni kutoa thamani ambao watu hao wanaihitaji, ambayo wanaikubali na kuwa tayari kuilipia. Kama bado hujatengeneza koneksheni za aina hiyo kwenye maisha yako, bado hujatoa thamani kubwa kwa wengine.

Utajiri na mafanikio yanayojengwa kwenye thamani yanadumu kuliko yanayojengwa kwenye uhaba au ulaghai. Kila uhaba una mwisho, kila ulaghai unagundulika, lakini thamani haipotei, kila wakati inahitajika hivyo anayeweza kuitoa ana uhakika wa kufanikiwa na kudumu kwenye mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha