2287; Katili isiyo katili…

Ukimuomba mtu kitu halafu akakataa, haijalishi amekupa sababu gani, unajisikia vibaya.
Maana mpaka unachagua kumuomba, ulijua kabisa ipo ndani ya uwezo wake.
Hivyo anapokataa inakufanya ufikirie mengi, labda hakupendi, hajali, ana roho mbaya na mengine.
Lakini kama wewe ni mkulima ambaye umepanda mazao yako na ukaomba sana mvua inyeshe halafu isinyeshe, hutalichukia anga au kujisikia vibaya, utaendelea kutegemea mvua itanyesha au utaendelea na mambo mengine.
Kadhalika ukianguka kutoka juu, ni nguvu ya mvutano ya dunia inayofanya uanguke, lakini hujawahi kuichukia au kuilaumu.
Inapokuja kwenye asili, huwa tunaichukulia ilivyo na kuangalia namna ya kuishi nayo.
Japo mambo ambayo asili inaweza kufanya ni ya kikatili, hujawahi kuiita asili ni katili.
Kama umepanda mazao kwenye kipindi cha msimu na mvua isinyeshe kisha yakakauka, huo ni ukatili mkubwa, lakini hujawahi kuuchukulia hivyo, badala yake unatafuta njia za kunyeshea au kusubiri msimu mwingine.
Ukiweza kuchukulia kila jambo kama unavyoichukulia asili, utakuwa na maisha tulivu kabisa.
Hakuna chochote kitakachokusumbua au kukukwaza, kwa sababu hakuna kitakachokuwa katili kwako.
Chochote ambacho watu wanafanya au kutokufanya kwako, chukulia kama ni asili inafanya, kukipokea na kisha kuangalia njia bora ya kukikabili.
Kila unachoona ni katili, kione kama asili inafanya yake na utaweza kuyaelewa mengi.
Tunajua kabisa sheria za asili huwa hazina huruma hata kama zinakuumiza, kama umeenda kinyume nazo hazitakuacha salama.
Ukiielewa asili, huwezi kuona chochote ni ukatili na hilo litafanya maisha yako yawe tulivu.
Kocha.