2289; Ulichozaliwa nacho, hupaswi kukiomba…

Jamii huwa haipendi uwe huru kuwa vile unavyotaka.
Na ili kukunyima uhuru wako, inahakikisha inakujengea aina fulani ya utegemezi ambapo utajiona bila jamii hiyo maisha yako hayawezi kwenda.
Ukianza na uhuru wenyewe, ulizaliwa ukiwa huru kabisa, lakini mamlaka mbalimbali zinajihamishia uhuru huo na kukufanya uzione hizo ndiyo zinakuweka huru. Uamini kwamba bila mamlaka hizo basi wewe haupo huru. Na mamlaka kubwa zinazoshikilia uhuru wa wengi ni dini na serikali. Mamlaka hizo zinajua ukijua uhuru wako hauzitegemei, hazitakuwa na nguvu ya kukutawala.
Ukienda kwenye upekee, wewe umezaliwa ukiwa wa kipekee kabisa, hajawahi kuwepo na hatakuja kuwepo mwingine kama wewe. Na hata kama mmezaliwa mapacha mnaofanana, bado kila mmoja ni wa kipekee.
Lakini jamii haitaki ujue na kuishi hivyo, na hapo imekuwa inakuweka kwenye kundi moja na wengine na kuhakikisha unashindana nao ili uwe kama wao.
Jamii inajua ukijitambua na kuwa wewe kwa utofauti wako, utakuwa wa gharama kubwa wakati jamii inakutaka uwe wa gharama ndogo au hata bure kabisa.
Furaha ni kitu kingine ulichozaliwa nacho, ambacho huhitaji masharti yoyote ili kukipata. Lakini jamii imewakamata wengi kwenye mtego wa kuamini bila watu au vitu fulani basi hakuna furaha.
Kufikiri ni kitu kingine ulichozaliwa nacho, huhitaji ruhusa ya yeyote kutumia akili yako kufikiri. Lakini jamii haitaki ufikiri, maana inajua ukifanya hivyo utahoji mengi na kuwa huru. Hivyo imekuwa inakulazimisha uamini au kufuata mkumbo na siyo kufikiri na kufanya maamuzi yako mwenyewe.
Niliyoshirikisha hapa ni mifano michache, lakini naamini picha umeipata na unaona vingi ulivyozaliwa navyo ambavyo jamii imekuwa inakupora na kukutaka uiombe ili ikupe kwa masharti.
Chochote ulichozaliwa nacho, ni chako kuwa nacho na hupaswi kukiomba kwa yeyote yule.
Ishi kwa msingi huu na maisha yako yatakuwa vile unavyotaka wewe na siyo wengine wanavyotaka uwe.
Seneca amewahi kusema mahitaji ya msingi ni machache na yako ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu, ni mahitaji ya anasa yanayotutesa.
Ukichagua kusimamia yale uliyozaliwa nayo, hakuna namna unaweza kuteseka.
Ndiyo, utakutana na magumu mengi, lakini kwa kuwa unajua unasimama wapi, hutasumbuka sana.
Kocha.