2293; Kuchezea Mfumo…

Sisi binadamu huwa tunatafuta mfumo wa kitu na kisha kuuchezea mfumo huo ili kujinufaisha sisi wenyewe zaidi.

Mji mmoja nchini India ulikuwa na tatizo la nyoka kuwa wengi, serikali ikaja na wazo la kununua nyoka ili kuwahamasisha watu kuwaua na kupeleka ili wapate pesa. Lengo ilikuwa ni kuwamaliza nyoka hao.
Lakini kilichoishangaza serikali, licha ya nyoka kutokuonekana tena mitaani, bado watu walikuja na nyoka ili walipwe.
Serikali ilipofanya uchunguzi, ikagundua kuna watu wameanzisha mradi wa kuzalisha na kufuga nyoka na wanawauzia wengine ambao wanawapeleka serikalini ili walipwe.

Huo ni mfano mmoja kati ya mingi ya jinsi gani sisi binadamu huwa tunatafuta kuuelewa mfumo na kisha kuuchezea ili kujinufaisha.

Hili limekuwa na madhara makubwa kwetu kuliko manufaa, kwani limekuwa chanzo cha kuingizwa kwenye utapeli na hata kupata hasara kubwa.

Fursa nyingi unazoona watu wanazihubiri saba kwamba zinalipa ni katika hali ya watu kujaribu kuuchezea mfumo.
Kile kilimo au ufugaji wa kwenye makaratasi, kwamba unaambiwa kilimo fulani kinalipa, ukilima heka moja inaingia miche kadhaa, kila mche unazalisha kiasi fulani. Ukikokotoa ni mamilioni ya pesa.
Ingia kwenye kilimo husika na matokeo yanakuwa tofauti kabisa.

Kadhalika uwekezaji unaoonekana kukua kwa kasi sana na wengi kuukimbilia, ukuaji wake hautokani na thamani, bali watu kufikiri wameshaujua mfumo na jinsi ya kuuchezea. Kinachokuja kutokea baadaye ni uwekezaji huo kuanguka na wengi kupoteza.

Jifunze kutambua mifumo ambayo watu wameshajua jinsi ya kuichezea na kuiepuka, maana haijalishi watu wananugaika kiasi gani, kinachokuja kutokea ni anguko.
Kinachofanya wengi kuanguka na mifumo hiyo ni kuona wengine wakinufaika na kutokutaka wapitwe.

Hakikisha kila unachofanya kinatoa thamani kwa wengine na watu hao wako tayari kulipia thamani hiyo.
Kama hakuna thamani unayozalisha, jua manufaa yoyote unayopata yanatokana na kuchezea mfumo na wakati utafika ambapo mfumo huo utaanguka.

Unapoambiwa unapanda fedha na baada ya muda unavuna mara mbili, huku hakuna mpango wowote wa jinsi gani fedha hiyo inazalisha faida hiyo kubwa shtuka, kuna mfumo unachezewa hapo.
Unapoambiwa kuna njia ya mkato na isiyohitaji kazi ya kufanikiwa jua ni mfumo unachezewa.
Kadhalika unapoambiwa kuna njia ya mkato ya kuwa na furaha, kama ilivyo kwenye kilevi, jua unakwenda kuchezea mfumo wa mwili kwa muda mfupi, ila baadaye mambo yatarudi kama yalivyokuwa.

Manufaa yoyote yanayopatikana bila kuzalisha thamani ni kucheza na mfumo na huwa hayadumu maana kila mfumo unaochezewa huishia kuanguka.
Epuka sana kuchezea mfumo au kujihusisha na mifumo iliyochezewa, manufaa yake huwa hayadumu kwa muda mrefu.

Kocha.