2318; Kitu rahisi kuahirisha…

Huwa tunajifunza sana kuhusu madhara ya tabia ya kuahirisha mambo.

Pale unapopanga utafanya kitu fulani halafu wakati wa kutekeleza ulichopanga unapofika hufanyi hivyo.

Tabia hii ni kikwazo kwa mafanikio ya wengi. Kwa sababu muda unapotea ambao hauwezi kurudi tena.

Kuna kitu kingine ni rahisi kuahirisha, lakini tumekuwa hatukipi uzito.

Kitu hicho ni kuahirisha kuishi, hapa ndipo wengi huyapoteza maisha yao bila hata ya kujua.

Kila wakati kwenye maisha kuna kitu unasubiri kipate au kikamilike ndiyo uanze kuishi.

Ukiwa masomoni utajiambia unasubiri uhitimu.
Ukihitimj utajiambia unasubiri upate kazi.
Ukipata kazi unajiambia unasubiri uwe na familia.
Ukiwa na familia unajiambia unasubiri ustaafu.
Ukishastaafu unajiona huna tena muda.

Hapo katikati bado kuna mengi yanajitokeza, kuumwa, kutokuelewana na watu, kupoteza na kadhalika.

Hitaji la kutaka kila kitu kiwe kimekamilika ndiyo uanze kuyaishi maisha yako ni kikwazo kikubwa kwako.

Namna pekee ya kuyaishi maisha yako ni kuyaanza kabla hata hayajakamilika utakavyo.
Kujua kwa wakati wowote na hali yoyote uliyonayo unaweza kuyaishi maisha yako.

Hakuna yeyote anayekuzuia isipokuwa wewe mwenyewe.
Acha kuwa kikwazo kwako mwenyewe, chagua sasa kuyaishi maisha yako kwa kuanzia hapo ulipo sasa ambapo panatosha kabisa.

Kocha.