2320; Unapowashauri wengine, unajishauri mwenyewe…
Watu wengi huogopa kutoa ushauri kwa wengine kwa kujiona hawajastahili kufanya hivyo.
Wengi hudhani ili uweze kutoa ushauri basi lazima uwe na uzoefu mkubwa kwenye eneo hilo.
Lakini hiyo siyo sahihi, unaweza kutoa ushauri hata kama huna uzoefu mkubwa kwenye jambo hilo.
Kwa sababu unapomshauri mtu mwingine, unakuwa umejishauri mwenyewe pia.
Kuna faida kubwa tatu unazozipata unapowashauri wengine;
Moja; kwa mtu kukuomba ushauri kunakufanya ujiamini, unaona kuna kitu cha kipekee amekiona kwako na ndiyo maaana amekuomba ushauri.
Mtu hawezi kukuomba ushauri kama hakuamini na wengine wanapokuamini unajiamini zaidi.
Mbili; unapotoa ushauri, inakusukuma ufikiri kwa kina kile unachomshauri mwingine hivyo hilo linakupa uelewa mkubwa kwenye kitu hicho.
Unaweza kuwa unadhani unajua kitu kwa undani, ila unapotakiwa kumweleza mtu mwingine unagundua unapaswa kupangilia vizuri.
Tatu; unapomshauri mtu kitu, inakulazimisha na wewe uishi kwa namna ulivyomshauri mwingine.
Utajiona ni mnafiki kama utamshauri mtu jambo fulani halafu wewe kufanya tofauti na ulivyomshauri.
Unapopata fursa ya mtu kukuamini na kukuomba ushauri usiipoteze, kwani siyo yeye tu anayenufaika, na wewe pia unanufaika.
Muhimu ni uepuke kutoa ushauri kwa watu ambao hawajakuomba, haitakuwa na msaada kwa yeyote.
Kocha.