2321; Usiyazungushe maisha…

Maisha ni magumu tayari, hivyo usiyafanye kuwa magumu zaidi ya halivyo.
Usiyazungushe sana maisha kwa vitu ambavyo viko wazi kabisa.

Kama kuna kitu unakitaka, kitake kweli na weka wazi kwamba unakitaka. Usilete michezo au mitego ukitaka wengine waweze kusoma mawazo yako wajue unataka nini. Wewe ndiye wa kuwaeleza na kusimamia kile unachotaka.
Kadhalika kwa vitu usivyotaka.

Umeiona fursa ya kufanya kitu fulani muhimu itumie mara moja. Usijicheleweshe ukaja kukuta fursa hiyo haipo tena. Kuna vitu muda wake ni mfupi, usiupoteze.

Utapunguza ugumu wa maisha kama utajijua wewe mwenyewe kiundani, kujua kile hasa unachotaka na kuweka wazi misingi unayosimamia.

Usidhani watu wataweza kusoma mawazo yako kwenye hayo na kisha kwenda na wewe ulivyo. Ni wajibu wako kuwajulisha hayo.

Kuwa mkweli kwako na kwa wengine pia, itapunguza usumbufu mwingi usio na lazima.

Kocha.