2323; Mambo ya kuzingatia wakati wa mabadiliko magumu…
Kila mtu huwa anapitia kipindi cha mabadiliko magumu kwenye maisha yake.
Ni katika vipindi hivyo ndipo wanaofanikiwa na wanaoshindwa wanapotengana.
Wanaofanikiwa wanavitumia vipindi vya mabadiliko vizuri, huku wanaoshindwa wakivitumia vibaya.
Haya ni mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa mabadiliko magumu ili yakupeleke kwenye mafanikio makubwa;
- Kujua uwezekano wa makubwa yanayoweza kutokana na mabadiliko hayo. Hapa unakuwa na picha nzuri ya matokeo bora yanayotokana ma mabadiliko magumu unayopitia.
-
Kutanua wigo wa faraja (comfort zone). Wigo wa faraja ni yale uliyozoea kufanya, ambayo hayakusumbui na yanakupa majibu ya uhakika. Unaupenda wigo huo kwa kuwa unakupa uhakika, japo ni kikwazo kwani matokeo yake huwa ni madogo. Wakati wa mabadiliko tanua wigo huo ili uwe tayari kujaribu mambo mapya na makubwa.
-
Kuelewa kiini cha mabadiliko na kujua mwenendo wa mambo mbalimbali kwenye maisha au kile unafanya. Kuna vitu huwa vinajirudia na kuna ambavyo huwa vinaongozana, kwa kujua mwenendo huo utaweza kuyafanya mabadiliko vizuri.
-
Kujenga jamii inayokuunga mkono na kukusaidia wakati wa mabadiliko. Huwezi kufanya kila kitu peke yako, unahitaji watu sahihi wa kuungana na wewe na kukusaidia wakati huo wa mabadiliko.
-
Kuwa tayari kukosolewa, kupingwa, kueleweka na kutambulika. Maamuzi mengi utakayofanya wakati wa mabadiliko hayataeleweka na kila mtu kwa sababu siyo kila mtu anaona kila unachoona wewe. Lazkma uwe tayari kukabiliana na hilo ili uweze kuyavuka mabadiliko vizuri.
Huwa tunapenda maisha yaende tutakavyo, kila kitu kiende kama tulivyozoea.
Lakini mambo yakiwa hivyo, hakuna ukuaji wala mafanikio.
Ukuaji na mafanikio ni matokeo ya mabadiliko makubwa ambayo huwa yanaumiza.
Kadiri unavyoweza kuyavuka mabadiliko hayo salama, ndivyo unavyofanikiwa zaidi.
Umejifunza hatua muhimu hapa, zifanyie kazi.
Kocha.