2327; Hatua tano za masoko…
Masoko ni sehemu muhimu ya biashara yoyote ambayo mtu anafanya.
Bila masoko hakuna wateja na bila wateja hakuna mauzo. Bila mauzo hakuna faida na bila faida hakuna biashara.
Hivyo unaweza kuona jinsi masoko yalivyo kiuongo muhimu kwenye biashara.
Wengi wanashindwa kwenye biashara kwa sababu hawana mpango mzuri wa masoko wanaofanyia kazi. Wengi hawana mpango kabisa na wale wenye nao haujapangiliwa vizuri kuleta manufaa.
Hapa tunakwenda kujifunza hatua tano muhimu za masoko unazopaswa kuzizingatia ili biashara inufaike.
Hatua ya kwanza ni kutengeneza kitu au huduma yenye manufaa kwa wengine ambayo watu wana uhitaji nayo. Bila ya kuwa na kitu chenye uhitaji, hata uwe na mbinu nzuri kiasi gani za mauzo, hazitakuwa na msaada kwa biashara.
Kwenye hatua hii ya kwanza lazima kile ulichonacho uweze kukitengenezea hadithi ya kuonesha thamani yake.
Hatua ya pili ni kutengeneza kitu hicho kwa namna ya tofauti kwa kulenga watu wa aina fulani. Ukitaka bidhaa au huduma iwe ya watu wote, inaishia kuwa haina mteja kabisa.
Lazima uchague wateja unaowalenga, wenye shida unayotatua na kisha kuandaa bidhaa au huduma yako kwa namna itawafaa hao.
Unapochagua watu unaowalenga na ukawaandalia kinachowafaa, itakuwa rahisi kuwashawishi.
Hatua ya tatu ni kutengeneza hadithi ambayo inahusisha unachouza na kuwagusa wateja uliowalenga. Hadithi hiyo lazima iguse maisha yao, iwafanye waone kitu hicho ni kwa ajili yao.
Hadithi iendane na imani na mitazamo ambayo kundi la watu uliowachagua tayari wanayo.
Hadithi ikiendana nao ni rahisi kushawishika kuliko kulazimisha watu wabadilike.
Hatua ya nne ndiyo ambayo wengi wanaijua na kuifanyia kazi, kusambaza habari njema za kile unachouza. Na hapa unafanya hivyo kwa kueleza hadithi yako kwa wale unaowalenga kwa namna itakayowashawishi nao kuendelea kueleza hadithi hiyo.
Hatua hii ni muhimu kwani ndiyo inafanya watu wajue uwepo wako. Lakini bila hatua tatu za mwanzo, hii haiwezi kufanya kazi vizuri.
Hatua ya tano ni muhimu zaidi lakini wengi huwa hawaijui au wanaipuuza. Hatua hiyo ni kujenga msimamo wa kuwepo na kutoa huduma bora kwa wateja miaka na miaka huku ukiendelea kuieleza hadithi.
Siyo wote watakaosikia hadithi yako mara moja watakuja, wengi wanahitaji kusikia mara nyingi ndiyo washawishike kununua.
Na wale wanaokuja kununua watarudi tena kama watapata kile walichotegemea.
Hivyo msimamo kwenye kutimiza ahadi, kutoa huduma bora na kuendelea kueneza hadithi ni muhimu mno.
Kwa kufuata hatua hizo tano, huku ukizitudia na kuziboresha kadiri unavyolisoma soko, utaweza kujenga wateja waaminifu kwa biashara yako na kuweza kupiga hatua.
Kocha.