2330; Nguzo Tano Za Kujijenga Binafsi…
Umekuwa unasikia sana ushauri wa kwamba kama unataka kufanikiwa kwenye maisha basi unapaswa kuwa wewe, unapaswa kuwa halisi kwako na siyo kuiga maisha ya wengine.
Kwa wengi ushauri huo huwa unaishia kuwachanganya badala ya kuwasaidia.
Hapa tunakwenda kujifunza nguzo tano za kujijenga binafsi.
Kwa kuzijua nguzo hizi tano, utajua maana halisi ya kuwa wewe na kuweza kuishi wewe ili ufanikiwe.
Nguzo ya kwanza ni kile unachothamini sana kwenye maisha yako. Kitu gani ukikikosa kwenye maisha unaona kama maisha hayana maana.
Achana na vile vitu vya nje, kuna vitu vya ndani yako ambavyo ukivikosa unaona kama maisha yamekosa maana.
Kuna ambao wakikosa uhuru binafsi wanaona maisha hayana maana.
Wengine wakikosa faragha yao wanaona dunia kama imeanguka, wakati wengine wakitaka hadhara zaidi.
Jua ni kitu gani unathamini zaidi kwenye maisha yako, kitu ambacho uko tayari kukisimamia kwa gharama yoyote ile.
Nguzo ya pili ni vitu unavyopenda kufuatilia. Hapa ni vile vitu vya nje yako ambavyo unapenda kuvifuatilia na pia unavijua kwa undani kuliko wengine. Yaani inapokuja kwenye vitu hivyo, huwa unahakikisha hupitwi kabisa.
Unajua tayari vitu gani unapenda kubifuatilia sana, vizingatie kwa kuwa ni muhimu.
Nguzo ya tatu ni vipaji ulivyonavyo. Hapa ni vile vitu ambavyo kwako ni rahisi kufanya wakati kwa wengine ni vigumu. Vile ambavyo kwako ni kama mchezo wakati kwa wengine ni kazi kubwa.
Kwa kujua vipaji vyako, unajua nguvu yako kubwa ilipo.
Nguzo ya nne ni matamanio makubwa uliyonayo. Kila mtu ana matamanio makubwa kwenye maisha yake, yanayomsukuma kufanya kila anachofanya.
Yajue matamanio makubwa uliyonayo, usikubali pale wengine wanapokukatisha tamaa kwamba hupaswi kuwa na matamanio makubwa.
Bila matamanio makubwa hakuna kikubwa kinachoweza kufanyika.
Nguzo ya tano ni sauti ya ndani. Kila mtu ana sauti ya ndani yake, ambayo inatoka ndani kabisa ya nafsi yake. Sauti hii inajua mengi na huwa inamtahadharisha mtu kabla ya hatari. Tatizo wengi huwa hawaisikilizi sauti hii na hata wanapoisikia huwa wanaipuuza.
Jifunze kuisikiliza sauti yako ya ndani na itakuwa mwongozo sahihi kwako.
Kwa kuzijua nguzo hizi tano kwako binafsi na kuziishi kwenye maisha yako, unakuwa moto wa kuotea mbali. Unakuwa na nguvu ya kufanya makubwa kwenye maisha yako na kuwashangaza wengi.
Kinachokutofautisha wewe na wewe na watu wengine ni mchanganyiko wa kipekee wa nguzo hizo tano.
Ukishaujua mchanganyiko huo, uishi kwenye kila siku ya maisha yako na hivyo ndivyo unavyokuwa wewe, unavyokuwa halisi kwako na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Unaposikia kuwa wewe, maana yake ni kuzijua na kuziishi nguzo hizo tano za maisha binafsi.
Kocha.