2332; Kupata Unachotaka…

Kutaka ni rahisi, kila mtu anataka kitu fulani kwenye maisha.
Kila mtu anataka fedha zaidi, anataka maisha mazuri zaidi na anataka kufanikiwa zaidi.

Lakini wachache ndiyo wanapata kile wanachotaka, huku wengi wakiwa hawana budi bali kukubali maisha ya kawaida ambayo ni ya chini kabisa.

Kuna hatua muhimu za kufuata ili uweze kupata kile unachotaka.

Kwanza ni kujua kwa hakika nini hasa unachotaka. Hapa lazima ukae chini na kuweka malengo ambayo yanapimika, yana hatua za kuchukua na muda wa ukomo ambapo lazima uwe umeyafikia.
Bila ya kuchambua kwa hakika nini unachotaka, ni vigumu kukipata.
Chukua mfano wa watu hawa wawili, mmoja anasema anataka kuwa tajiri, mwingine anasema miaka kumi kutoka sasa nataka nifikie kiasi cha bilioni 2 kupitia uwekezaji kwenye majengo.
Najua unajua katika hao wawili nani ana nafasi kubwa ya kupata anachotaka.

Pili ni kupangilia muda wako na kuweka vipaumbele vyako vizuri.
Kama ambavyo wengi husema, mambo mengi muda mchache. Tunachojua ni hatutakuja kupata muda wa ziada. Hivyo njia pekee ni kutumia vizuri muda tulionao, kwa kuweka vipaumbele vyetu vizuri kulingana na malengo yetu.
Kama hakuna vipaumbele tulivyojiwekea, kila kitu kinakuwa kipaumbele kwetu, tunahangaika kila siku, tunachoka sana ila hakuna hatua tunazopiga.

Tatu ni kuwa mtu wa shukrani. Lawama na malalamiko ni adui wa kuchukua hatua na kufanikiwa. Badala ya lawama na malalamiko, unapaswa kuwa mtu wa shukrani. Unapaswa kushukuru kwa kila jambo, liwe zuri au baya kwa sababu kila linalokuja kwako, linakuja kwa kusudi maalumu.
Unapokuwa mtu wa shukrani unajiweka kwenye nafasi ya kupata mazuri zaidi, maana unakuwa umeiambia asili ikufungulie baraka zake zaidi.

Nne ni imani isiyotikisika kwamba utapata unachotaka. Safari ya kufikia malengo yako haitakuwa rahisi, utakutana na magumu ya kila aina. Kama hutakuwa na imani kali ni rahisi sana kukata tamaa kwenye hii safari.
Pamoja na yote utakayokuwa unapitia, imani yako kwamba lazima utafanikiwa kufikia malengo yako haipaswi kutikisika hata kidogo. Hata pale wengine wote wamekata tamaa juu yako, endelea kujiamini na kuamini utapata unachotaka.
Hata kama huoni njia ya kufika unakotaka, endelea kuamini. Kama umewahi kusikia imani inaweza kuhamisha milima, basi jua hilo ni kweli.
Katikati ya giza zito na ukiwa hujui unatokaje, kwa imani yako kali, asili inafungua milango yake na unapata mpenyo wa kufika unakotaka kufika.

Tano ni kuhakikisha unaendelea kuwa hai na kwenye mapambano mpaka utakapokutana na mpenyo wako.
Wale waliofanikiwa kupata wanachotaka, huwa tunaona kuna bahati fulani wamekutana nazo kwenye maisha. Tukiona hivyo tunadhani mafanikio yao yameletwa na bahati hizo.
Ukweli ni kwamba mafanikio yao yametokana na wao kuwa hai na kwenye mapambano mpaka bahati zikawakuta.
Hapa unapaswa kuepuka sana hatari zote ambazo zitakuondoa kabisa kwenye mapambano.
Jua kila mtu ana nafasi ya kukutana na bahati nzuri kwenye maisha yake, lakini ni kama atakuwa kwenye mapambano kwa muda mrefu.
Wengi huondoka kwenye mapambano kabla bahati zao hazijawafikia.

Sita ni kuambatana na rafiki wa kweli ambaye ni kazi. Kupanga ni rahisi, kutekeleza ni kugumu. Wewe penda kazi, weka kipaumbele kwenye kazi, amini na weka kazi.
Ukichanganya kazi na hivyo vingine, hakuna kitakachokushinda.

Saba ni muda, uvumilivu na ung’ang’anizi. Unajua kabisa mambo mazuri hawahitaji haraka, hivyo acha kukimbizana na njia za mkato na jipe muda.
Unaweza kufanya kila unachopaswa kufanya lakini matokeo yakachelewa, lazima uwe na uvumilivu.
Wakati mwingine matokeo yanakuja tofauti kabisa na ulivyotegemea, lazima uwe king’ang’anizi kwa unachotaka na usikubali kupokea kingine chini cha hicho.

Kama bado hujapata unachotaka, siyo kwa sababu huwezi au kwa sababu huna bahati, bali kwa sababu labda bado hujawa kwenye mchakato au kama uko kwenye mchakato basi wakati wako bado.
Endelea kuamini, endelea kuweka kazi, kwa wakati usiotegemea, asili itafungua milango yake na utapata mpenyo mkubwa.

Kocha.