2333; Ili Kubaki Hapo Ulipo…
Dunia inakwenda kasi sana,
Kama unataka kubaki hapo ulipo, lazima uende na kasi ya dunia.
Na kama unataka kwenda zaidi ya ulipo sasa, lazima uizidi kasi ya dunia.
Kwenye maisha hakuna kusimama, kuna kwenda mbele au kurudi nyuma.
Kubali hapo ulipo ni kuchagua kurudi nyuma kwa sababu dunia haisimami, inaendelea kwenda mbele.
Teknolojia zinakua kwa kasi, mambo yanabadilika sana, kutokubadilika kwa kasi hiyo ni kuchagua kupotezwa.
Kila unapojiambia kwamba umeridhika na ulipo sasa, jikumbushe dunia iko kasi na inakuacha nyuma.
Hivyo kama unataka ubaki na hapo uliporidhika napo, lazima ubadilike na dunia inavyobadilika.
Chagua kubadilika au kuachwa nyuma, dunia haikusubiri wewe uwe tayari, inaendelea kwenda na mipango yake. Ni wajibu wako kuona jinsi dunia inavyobadilika ili na wewe ubadilike pia.
Na kubadilika siyo mara moja na kuwa umemaliza kila kitu, mabadiliko ni zoezi endelevu.
Huwa kuna kichekesho cha mtu analalamika kwamba kila akipata ufunguo wa maisha watu wanabadili kitasa.
Hivyo ndivyo mabadiliko yalivyo pia, ukishabadilika kuendana na mabadiliko yaliyopo, mabadiliko mapya yanakuja na unapaswa kubadilika tena.
Kocha.