2338; Maisha Kama Kombolela…
Kama unaukumbuka mchezo wa kombolela, una siri kubwa sana ya mafanikio kwenye maisha.
Japo hatukuwa tunajua funzo lililo kwenye mchezo huo wakati tunacheza.
Katika kucheza mchezo huo, kama wewr ndiye unayewatafuta wengine, kwanza lazima uwajue wote wanaoshiriki kwenye mchezo.
Ukishawajua, lazima uwe na viashiria vya wapi watu hao wanaweza kujificha.
Huwezi tu kutafuta kila mahali, utaenda mbali sana na aliye karibu atakuja kuwakomboa ambao umeshawaona.
Hivyo mkakati wako inabidi uanze na viashiria vya wapi watu fulani wanaweza kujificha, kisha kufuata viashiria hivyo mpaka uwapate wote.
Ukiwa mzembe kwa kutokujua viashiria vya wapi watu wanaweza kuwa wamejificha, utaishia kuwa mtafutaji mara zote.
Hapo kuna funzo kubwa sana kuhusu mafanikio kwenye maisha. Mafanikio unayoyataka tayari yapo kwenye dunia, na wewe unayatafuta. Kama hujui viashiria vya wapi mafanikio yako yapo na uende kuyatafuta hapo, maisha yako yote utakuwa mtu wa kutafuta na hutapata.
Lazima uwe na viashiria, na kikubwa mabisa ni kujua kusudi lako, vipaji vyako na yale unayopendelea kufanya.
Kisha kujua mahitaji makubwa ambayo wengine wanayo na unaweza kuwatimizia kwa vipaji na uwezo wako.
Bila kujua viashiria hivyo, utahangaika na maisha ila hakuna utakachopata. Kila unapokaribia kupata unachotaka, kopo linapigwa na inabidi uanze tena upya.
Kwa chochote unachotaka kwenye maisha jua kiashiria chake na fuata hicho, lazima utakipata.
Ukisikiliza nafsi yako na kuiamini, utaviona viashiria vingi.
Lakini kama utaipuuza, utakimbizana na mengi na hutapata unachotaka.
Maisha ni kombolela, jua viashiria vya mafanikio yako viko wapi, nenda hapo, weka juhudi na utafanikiwa.
Kocha.