Rafiki yangu mpendwa,
Leo nataka niwe mtabiri wako.
Unakumbuka ile siku ambayo ulisoma makala nzuri sana na kujiambia mwandishi alikuwa ananilenga mimi kabia.
Au siku uliyosoma kitabu na kujiambia ulikuwa wapi siku zote hujakisoma na kupata hayo mazuri.
Au ile siku uliyohudhuria semina na kusikia shuhuda za wengine wakifanya makubwa na wewe ukakata shauri kwamba lazima ufanye makubwa?

Ukatoka ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kufanya makubwa kwenye maisha yako pia.
Siku hiyo ukakosa hata usingizi, usiku kucha ukawa unaweka mipango na kuona jinsi maisha yako yanavyokwenda kubadilika kabisa.
Hamasa inakusukuma na unaanza kuchukua hatua kama ulivyopanga.
Lakini siku chache baadaye, unajikuta umerudi kwenye mazoea yako, hamasa yako imeisha kabisa na hufanyi tena yale uliyopanga kufanya.
Hata ukikumbuka hamasa uliyokuwa nayo unaona kama ulikuwa unajidanganya, ni kitu kisichowezekana. Kwa kujiambia hivyo unaona ni sahihi kurudi kwenye mazoea.
Leo nakuambia siyo sahihi kurudi kwenye mazoea, nakuambia inawezekana kabisa kufanya chochote unachotaka na inawezekana kuleta mabadiliko yanayodumu na kuwa na hamasa isiyoisha.
Na hapa ni njia za kuweza kufanya hivyo.
1. Jua nini unataka na kwa nini unakitaka.
Hatua ya kwanza kwenye kuleta mabadiliko yanayodumu kwenye maisha yako ni kujua nini unataka na kwa nini unakitaka.
Wengi wanapata hamasa kubwa ya kufanikiwa, lakini hawajui mafanikio kwao ni nini.
Na hata wakiyajua, hawana kwa nini kubwa inayowasukuma.
Ndiyo maana ni rahisi watu kuhangaika na mambo mengi na yasiyo na tija kwao.
Ukishajua nini hasa unachotaka, maana yake unaachana na vingine vyote visivyohusiana na hicho. Kama bado unahangaika na mengi, hujajua hasa unachotaka.
Kujua kwa nini unataka unachotaka ni muhimu kwa sababu safari ya kukipata haitakuwa rahisi, utakutana na vikwazo na changamoto nyingi.
Kujua kwa nini unataka unachotaka kutakusukuma uvuke vikwazo na changamoto zote mpaka ukipate.
Kwa nini kubwa ndiyo nguvu ya kuleta mabadiliko yanayodumu kwenye maisha yako.
Jua unachotaka na jua kwa nini unakitaka kisha pambana kukifikia.
2. Kuwa wewe, usiige yeyote.
Kusikia wengine wamefanikiwa kwenye kitu fulani haimaanishi na wewe unaweza kufanikiwa kwenye kitu hicho pia.
Na hapa ndipo wengi hupotea, mtu anasikia ushuhuda wa mtu aliyefanikiwa kwenye ufugaji na yeye anaenda kufanya ufugaji, anasikia mwingine kufanikiwa kwenye kilimo na yeye anaenda kulima.
Hadithi za mafanikio ni nyingi kama daladala kwenye kituo cha magari, lakini siyo zote zinaweza kukufikisha unakotaka, japo zitawafikisha wengine wanakokwenda.
Lazima ujue daladala sahihi kwako ndiyo uweze kufika unakotaka kufika.
Unachopaswa kujifunza kwenye hadithi za mafanikio ya wengine ni imani, mitazamo na misingi ambayo wamekuwa wanaiishi.
Kuiga wanachofanya waliofanikiwa hakutakuwezesha kufanikiwa kama wao. Lazima ujitambue wewe mwenyewe kisha kupambana kuwa wewe.
Usimuige mtu mwingine yeyote, ndani yako una uwezo wa kipekee, ukitumia huo na misingi ya mafanikio unayojifunza, utaweza kufanya kitu cha tofauti kabisa na ukafanikiwa sana.
Jisikilize mwenyewe na kazana kuwa wewe, kuwa tofauti na kusimamia misingi sahihi. Utapata matokeo mazuri ambayo yatakufanya uendelee kubaki kwenye njia yako.
Ukiiga wengine na usipate matokeo kama yao, itakuwa rahisi kukata tamaa na kuishia njiani.
3. Jenga tabia.
Hamasa ndiyo inakufanya uanze safari ya mafanikio, lakini tabia ndiyo zinakufanya ubaki kwenye safari hiyo.
Hamasa ni ya kuja na kuondoka, tabia ni kitu kinachodumu.
Jijengee tabia ambazo zitakufikisha kwenye mafanikio yako, kwa kuwa na hatua ubazochukua kila siku ya maisha yako bila kuacha.
Kama unafanya biashara, kila siku fanya kitu cha tofauti kwenye biashara hiyo.
Kama ni kazi kila siku jifunze na kuchukua hatua bora zaidi.
Jijengee tabia ya kufanya kila siku yale ambayo yanakufikisha kwenye mafanikio yako na usiache hata siku moja kufanya.
Ikishakuwa tabia kwako, utajikuta unafanya bila ya kutegemea hamasa.
Ikishakuwa tabia kwako, siyo rahisi kuacha na kuishia njiani.
4. Usifanye kwa pupa.
Umewahi kupata hamasa ya kufanya mazoezi na siku ya kwanza ukafanya kwa kiwango kikubwa? Nini kilitokea kwenye siku zilizofuata? Hukuweza kufanya tena mazoezi.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio. Unaweza kusikia shuhuda za waliofanikiwa kwamba wanaamka saa 9 alfajiri kila siku. Wewe ukatoka na hamasa kubwa na kutaka uanze kuamka saa 9 alfajiri kila siku.
Kinachotokea ni unachotaka sana na kushindwa kuendelea.
Haijalishi una hamasa kiasi gani, usianze kwa pupa, bali anza kidogo kidogo na piga hatua kukua zaidi.
Kwa mfano huo wa kuamka, kama umekuwa unaamka saa 12 asubuhi, anza kwa kuamka saa 11 na nusu, fanya hivyo mpaka uzoee, kisha amka saa 11 kamili, endelea hivyo mpaka ufike muda unaotaka.
Kwa mabadiliko yoyote unayotaka kufanya, usiyaendee kwa pupa, bali nenda nayo hatua kwa hatua.
Mwili wako umeshajijengea mazoea yake ambayo ukiyavunja mara moja unaushtua sana na hivyo hauwezi kuhimili.
Nenda kwa hatua, huhitaji ushujaa wa kufika kwenye kilele mara moja, bali unahitaji kujenga msingi utakaofanyia kazi muda mrefu.
5. Zungukwa na watu sahihi.
Haijalishi una hamasa kiasi gani, kama utaendelea kuzungukwa na wale uliokuwa unazungukwa nao, ambao wengi wanaishi kwa mazoea na wamejikatia tamaa, hutaweza kudumu kwenye mabadiliko hayo.
Wanaokuzunguka wana nguvu kubwa ya ushawishi kwako, wakiona unabadilika hawatakuacha kirahisi, watakurudisha kwenye mazoea.
Unapobadilika, chagua watu wanaoishi kwa mabadiliko uliyoyafanya na ambatana nao. Hawa watakupa matumaini na kukusukuma zaidi.
Ni vigumu kukata tamaa ukiwa umezungukwa na wanaopambana. Utajiuliza kwani wao wanaweza wana nini na mimi nishindwe nina nini.
Ni muhimu sana uzungukwe na watu sahihi, hasa kipindi cha mwanzo cha mabadiliko yako, maana hao ndiyo watakufanya ubaki kwenye mabadiliko uliyofanya.
Kama bado hujawa kwenye KISIMA CHA MAARIFA basi itakuwa vigumu sana kwako kudumu kwenye mabadiliko. Chukua hatua ya kujiunga na KISIMA leo hii ili uwe kwenye jamii sahihi kwa mafanikio yako. Wasiliana na 0717 396 253 kupata maelekezo ya kujiunga.
6. Endelea kuchochea hamasa.
Huwa huli chakula mara moja na kusema umeshiba milele, kila siku lazima ule.
Huwa huogi mara moja na kujiambia umetakata milele, kila siku lazima uoge.
Sasa inashangaza unaposoma makala au kitabu kimoja, unapata hamasa na kuona umeshamaliza kila kitu.
Hapo unajidanganya na kujiweka kwenye hatari ya kuishia njiani.
Unapaswa kuendelea kuchochea hamasa yako kila siku kwa kuendelea kujifunza bila kuchoka au kuona umeshajua kila kitu.
Kila siku jifunze vitu vipya na vinavyokusukuma kupiga hatua zaidi.
Kuendelea kuchochea hamasa yako ya kufanikiwa, kila siku tembelea www.amkamtanzania.com
Pia jipatie vitabu vya kusoma kila siku kama TABIA ZA KITAJIRI, UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na BIASHARA.
Kupata vitabu hivyo na vingine vizuri wasiliana na 0752 977 170 au fungua www.somavitabu.co.tz
Rafiki, kubadilika ni tukio, kubaki kwenye mabadiliko ni mchakato. Mafanikio siyo tukio bali mchakato hivyo jenga mchakato sahihi utakaokufanya udumu kwenye mabadiliko na uweze kupata mafanikio makubwa.
Kocha Dr Makirita Amani.