2350; Uhalisia hauna mbwembwe…
Angalia kipindi cha mapishi kwenye tv au mtandaoni.
Kisha nenda kapike kwa hatua zote ulizojifunza kwenye kipindi hicho.
Matokeo ya mwisho hayatakuwa kama unayoona kwenye tv.
Kuna mahali utakosea tu, hata kama ni kidogo kiasi gani, labda ni chumvi utazidisha au kupunja, au mafuta yasitoshe au maji kuzidi.
Unapoangalia kwenye tv au mtandaoni, wewe unayaona matokeo ya mwisho, huoni mchakato.
Unapata picha kwamba wao ni wakamilifu katika kufanya hayo ila wewe ndiyo siye mkamilifu.
Unachosahau ni kwamba unapoangalia kwenye tv, unayaangalia matokeo ya mwisho na siyo mchakato.
Wakati kipindi kinaandaliwa, kuna makosa mbalimbali yalifanyika, lakini hayo hutayaona kwenye kilindi cha mwisho.
Hivyo wewe unapopata matokeo ya tofauti haimaanishi huwezi au hufai, huo ndiyo uhalisia, ndivyo maisha yalivyo, hakuna anayepatia kwenye kila analofanya.
Mitandao ya kijamii ndiyo imezidi kuharibu hilo. Kwenye mitandao hiyo kila mtu ana maisha mazuri na yenye furaha muda wote.
Muda mwingi wako kwenye starehe na wanaonekana kuyafaidi maisha.
Wakati unaangalia picha hizo za wengine unazilinganganisha na maisha yako, ambayo unayajua kwa uhalisia kuliko unavyoyajua ya wengine, unayaona hayajakamilika kama ya wengine.
Unachosahau ni kwamba kuna mambo mengi huwa unayaona kwenye maisha ya kawaida ya watu ila kwenye maisha ya mitandaoni ni nadra kuyaona.
Hilo linaashiria ni jinsi gani maisha ya mitandaoni yalivyo ya kuigiza na yanayotofautiana kabisa na uhalisia.
Kama unachoona kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandaoni kinapishana na uhalisia, amini zaidi unachoona kwenye uhalisia kuliko unachoona kwa vyombo vingine.
Maana uhalisia hauna mbwembwe kama unazoweza kuona kwenye vyombo mbalimbali.
Kamwe usiyalinganishe maisha yako halisi na yale unayoona kwenye vyombo vya habari na mitandao. Ambacho huoni kwa uhalisia siyo ukweli kwa asilimia 100, kuna mbwembwe nyingi zimeongezwa.
Ndiyo maana hata baadhi ya hadithi za waliofanikiwa zimekuwa hazina manufaa kwa wengi, kwa sababu zina mbwembwe nyingi zisizoendana na uhalisia.
Uangalie uhalisia, achana na mwembwe.
Kocha.
Asante kocha
LikeLike
Karibu Alex
LikeLike