2360; Unakokimbilia Ni Wapi?
Ni rahisi kujikuta ukiharakisha mambo unayoyafanya, lakini umewahi kujiuliza unakokimbilia ni wapi?
Hebu fikiria mtu anayeharakisha kufanya kazi yake, anashindwa hata kuifanya kwa umakini, halafu anakokimbilia ni kwenda kubishana.
Au fikiria mtu anayeharakisha kumhudumia mteja kwenye biashara, anaharakisha mteja aondoke, ili tu aingie kwenye mitandao na kufuatilia yanayoendelea.
Hebu jiulize hili swali kila unapojikuta unaaharakisha chochote unachofanya. Jiulize kipi muhimu, unachofanya sasa au kile unachokwenda kufanya kwa kuharakisha cha sasa.
Mara nyingi mno utajikuta unaharakisha kilicho muhimu, kukimbilia kile ambacho hakina umuhimu wowote.
Mtu mmoja amewahi kusema maisha ni kile unachopoteza wakati unaharakiaha kufanya vitu.
Haishangazi kwa nini mtu anaweza kuja kushtuka ni miaka 10 amefanya kazi ila haoni cha tofauti alichofanya.
Kwa sababu alikuwa akiharakisha tu, kukimbilia yasiyo na umuhimu.
Sasa wewe achana na hilo la kuharakisha.
Kwanza kabisa weka vipaumbele vyako vizuri, chagua kufanya yale tu ambayo ni muhimu na yenye mchango kwako kufikia ndoto zako.
Kisha unapofanya kitu, weka umakini wako wote hapo. Usifanye kwa kuharakisha kama hakuna cha muhimu zaidi unachokimbilia.
Hapa namaanisha kama una wateja wengi inabidi uwahudumie, basi unapaswa kwenda kasi ili wote wapate huduma.
Lakini kama una mteja mmoja tu mbele yako, mpe umakini wako wote, mpe muda wa kutosha ili umhudumie vizuri.
Kwa kufanya hivyo utamgusa zaidi kila mteja unayemhudumia na kujenga sifa nzuri kwa wateja wako.
Usiharakishe yaliyo muhimu, ili kwenda kufanya yasiyo muhimu. Chagua machache muhimu ya kufanya na weka umakini wako wote katika kuyafanya.
Kocha.