2361; Kama Bado Unajiuliza, Jibu Ni Hapana…
Kama bado unajiuliza kama una furaha au la, jibu liko wazi, huna furaha.
Wenye furaha hawapotezi muda kujiuliza kama wana furaha au la, bali wanayafurahia maisha yao.
Kama bado unajiuliza kama mtu anakupenda au la, jibu unalo, hakupendi. Upendo ukiwepo huwa uko wazi na siyo wa kutafuta.
Kama bado unajiuliza kama umefajikiwa au la, jibu pia unalo, bado hujafanikiwa. Ukifanikiwa unajua tu, huna haja ya kujiuliza.
Vitu bora kabisa kwenye maisha viko wazi, havihitaji ujiulize au ujichunguze sana.
Tatizo ni kwamba hata unapojiuliza maswali hayo, hutafuti majibu ya uhakika, bali unatafuta usumbufu wa kukuondoa kwenye maswali hayo.
Badala ya kujibu kwa nini huna furaha, unakimbilia kutumia vilevi kwa kuona vitakupa furaha.
Badala ya kujibu kwa nini hujafanikiwa na kutafuta njia ya mafanikio, unakimbilia kushabikia mafanikio ya wengine.
Tafakari leo ni maeneo gani ya maisha yako bado unajiuliza maswali, kisha tafuta majawabu ya uhakika na siyo kutafuta usumbufu.
Kila eneo la maisha yako ambalo bado una maswali nalo, tafuta majawabu ya uhakika na hakikisha huyakimbii maswali.
Lakini pia tambua kuwa na maswali haimaanishi maisha yako hayajakamilika, bali inamaanisha unatambua hujafika pale unapotaka kufika na hapo unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuelekea huko.
Kama bado unajiuliza, jibu ni hapana na anza kuchukua hatua mara moja ili kupata majawabu ya uhakika.
Kocha.