Rafiki yangu mpendwa,
Nenda kwenye kituo chochote cha mabasi, mfuate dereva aliye ndani ya basi linalotaka kuondoka na muulize hilo basi linaelekea wapi?

Bila ya kufikiria mara mbili, atakujibu moja kwa moja ni wapi basi hilo linakwenda. Na kwa asilimia 99.9 basi hilo litafika kule linapokwenda.

Na hiyo ni kwa sababu moja, dereva haondoki kwenye kituo cha basi akiwa hajui basi analoendesha linaelekea wapi.

Sasa turudi kwako na swali hilo hilo. Ndiyo unaamka asubuhi na kuwahi kwenye kazi au biashara zako.
Lakini je mtu akikusimamisha mara moja na kukuuliza unaenda wapi na maisha yako unaweza kumjibuje?

Kwa ninavyowafahamu wengi, hawana jibu la moja kwa moja. Itawachukua muda kuanza kufikiria nini hasa wanataka. Na hata wakishajua wanachotaka, bado hawajiamini kusema wapi maisha yao yanaenda na wanajiona wakifika wapi.

Hebu fikiria umeenda kituo cha basi, ukakata tiketi ya kutoka Dar kwenda Dodoma, ukaonyeshwa basi unalopaswa kupanda. Basi linaondoka ila dereva anazunguka tu eneo moja, unaona muda unaenda na safari haielekei kwenye njia sahihi.
Unaamua umuulize dereva kwani kuna nini? Anakujibu hajui hilo basi linaenda wapi, yeye ameambiwa tu aendeshe.
Je utaendelea kukaa ndani ya basi hilo?

Jibu ni hapana, utakasirika na kushuka haraka. Ulishaeleza wapi unaenda lakini hujawekwa kwenye basi sahihi.

Sasa fikiria kwa kitu kidogo kama safari unaweza kukasirishwa hivyo, vipi kwa hatima ya maisha yako?
Unaamka kila siku mapema, unaweka juhudi kwenye shughuli zako siku nzima, unaimaliza siku ukiwa umechoka kweli kweli.
Lakini cha kushangaza, hujui maisha yako yanaenda wapi!

Na pale ambapo maisha unayoenda nayo hayakuridhishi, badala ya kukaa chini na kujisikiliza ili ujue kipi hasa unachotaka, unakimbilia kwenye usumbufu.
Unatumia vilevi ili usahau shida zako kwa muda.
Unakuwa shabiki mkubwa wa mchezo, ili timu unayoshabikia inaposhinda ujione na wewe umeshinda.
Au unazurura mitandaoni na kuwashambulia wale wanaojua wapi wanaenda kwa kujiona wewe uko sahihi kuliko wao.

Hizo ni dalili chache kati ya nyingi za wale ambao wako mbio kweli na maisha, ila hawajui yanawapeleka wapi.

Rafiki yangu, nimeona wengi wakiteseka na maisha ya aina hiyo na baadaye kuja kuyajutia sana.
Na nimejipa wajibu wa kuhakikisha kila anayetaka basi hapotezi muda wake kuhangaika na yasiyo sahihi.

Kupitia KISIMA CHA MAARIFA, nimejipa majukumu makubwa mawili, kila anayejihusisha na mimi ni lazima alijue kusudi la maisha yake na kuliishi na awe na ndoto kubwa anazopambana kila siku kuzifikia.

Ni hayo mawili tu, KUSUDI na NDOTO, ambayo baada ya kufanya utafiti kwa muda mrefu, nimegundua yanaweza kubadili maisha ya mtu yeyote yule, bila kujali anaanzia wapi.

Mtu akilijua kusudi la maisha yake hawezi kupoteza muda wa maisha yake kuhangaika na yasiyo sahihi kwake.
Mtu akiwa na ndoto kubwa, hawezi kuishi maisha ya viwango vya chini na ya mazoea.

Mhamasishaji Eric Thomas anasema mchukue mtu yeyote unayeona ni mvivu na hawezi kufanya chochote. Mpeleke kwemye kina kirefu cha maji kisha mzamishe kwa nguvu. Ghafla utamuona ni mtu mwenye juhudi kubwa kabisa za kujiokoa kutoka kwenye maji hayo.
Hapo ni kwa sababu ana kusudi moja tu, kuhakikisha hafi. Atapata nguvu za kila aina kujiokoa asife kwenye maji hayo.

Hiyo ndiyo nguvu iliyolala ndani ya walio wengi, ambao kwa nje tunawaona kama wamepotea.
Kama wakiweza kulijua kusudi kubwa la maisha yao, hawawezi tena kupoteza au kuharibu maisha yao.

Hili ni jambo muhimu mno, lakini kwa nini wengi hawalifanyi?
Jibu ni kwa sababu siyo rahisi.

Ukienda kununua simu mpya, ndani ya boksi la simu kunakuwa na kijitabu cha jinsi ya kutumia simu hiyo. Kitabu kinaeleza uwezo wa simu na mambo gani unaweza kufanya kwa kutumia simu hiyo.

Lakini mtoto mchanga anayezaliwa, haji na kitabu kinachoeleza matumizi yake na uwezo mkubwa ulio ndani yake.
Hivyo wazazi wanamlea kwa kubahatisha, jamii inamweka kwenye mfumo wa elimu na malezi ambao unafuta kabisa kile cha kipekee kilicho ndani yake na anaishia kulinganishwa na wengine.

Mpaka anakuwa mtu mzima, anakuwa ameshajisahau, hawezi tena kujisikiliza bali anafuata kila ambacho jamii inataka kwake.
Hivyo ndivyo ulivyofika hapo ulipo sasa.

Pamoja na hayo yote, bado lipo tumaini.
Haijalishi umefika wapi, lipo tumaini kwako kuyabadili maisha yako sasa, kuacha kuyapoteza na kuishi kwa namna ambayo utaacha alama hapa duniani.
Uweze kujisikiliza, kujitambua na kuishi kwa uhalisia wako, ili uweze kufanya makubwa hapa duniani.

Tumaini hilo lipo kwenye kujua KUSUDI LA MAISHA YAKO na kuwa na NDOTO KUBWA UNAZOZIPIGANIA.

Kama una mfumo unaokuwezesha kutambua vitu hivyo vikubwa viwili na ukaviishi, basi ufanyie kazi mfumo huo.
Lakini kama huna mfumo huo, kama mpaka sasa umekuwa unahangaika na maisha yako na huoni hatua unazopiga, kubali kwamba unahitaji msaada.

Hakuna yeyote ambaye amewahi kupiga hatua kwenye maisha na kufanya makubwa bila ya msaada.
Ni mwanasayansi Einstein aliyenukuliwa akisema kama nimeweza kuona mbali zaidi, ni kwa sababu nimesimama kwenye mabega ya walionitangulia.

Angalia wale ambao wameweza kuacha alama kubwa kwenye maisha na jifunze kwao, kama utapata unaoweza kujifunza kwao moja kwa moja itakuwa vizuri.
Kama huwezi kupata wa moja kwa moja basi angalau soma vitabu vinavyowahusu
Na kwa dunia ya sasa, huna kikwazo chochote kwenye kujifunza, ni wewe tu useme hutaki.

Lakini pia ungana na wale walio kwenye safari ya kuishi kusudi la maisha yao, wale wanaojua maisha yao yanakwenda wapi na hawapotezi tena muda kuhangaika na yasiyo muhimu.
Kwenye jamii zetu siyo rahisi kuwapata watu wa aina hii, ila wapo, ukiwatafuta utawapata.

Lijue kusudi la maisha yako, uko hapa duniani kufanya nini.
Kuwa na ndogo kubwa unazozipigania, hizo zinakupa mwelekeo wa maisha yako.
Kwa kuwa na hivyo viwili, unakuwa moto wa kuotea mbali, maisha yako yataacha alama kubwa hapa duniani.

Rasilimali muhimu.

Kama nilivyokushirikisha hapo juu, safari hii ya kuyaishi maisha yako haitakuwa rahisi, kwa sababu kwa miaka mingi umekuwa unaishi maigizo.
Hapa kuna rasilimali muhimu zitakazokusaidia kama utachagua safari hii.

1. Kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA. Ndani yako kuna nguvu kubwa ambayo imelala, ukiitambua na kuweza kuitumia, itafanya makubwa mpaka utajishangaa mwenyewe.

2. Kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI. Ili uweze kuweka umakini kwenye maisha yako, lazima uondokane na usumbufu unaokuzunguka sasa. Simu janja na mitandao ya kijamii ni kikwazo kikubwa kwako. Kupitia kitabu hicho utaweza kuondoa usumbufu huo na kuweka umakini kwenye kuyaishi maisha yako.

Kupata vitabu hivi, wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa vitabu ulipo.

3. Kundi la KISIMA CHA MAARIFA. Rasilimali ya tatu na muhimu unayoihitaji sana ili uweze kuyaishi maisha yako ni kuwa kwenye kundi la KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni jamii ya tofauti na ya kipekee kabisa katika kuyaishi maisha halisi na ya mafanikio makubwa. Kwa kuwa ndani ya jamii hiyo unapata mafunzo na usimamizi wa karibu katika kuishi kusudi lako na kupambania ndoto zako kubwa.

Kupata nafasi kwenye jamii hii, tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717 396 253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA.

Rafiki, usikubali kupita hapa duniani kama msindikizaji. Hakikisha kuna alama unaiacha hapa duniani. Tayari una kila unachohitaji ili kuacha alama hiyo. Ni wewe kuamua kuchukua hatua sasa.
Hapa umejifunza ya msingi, chukua hatua sasa kabla maarifa haya uliyoyapata hayajapoa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani,
www.amkamtanzania.com