Rafiki yangu mpendwa,
Hukuja hapa duniani kwa bahati mbaya, bali umekuja kwa kusudi maalumu, ukiwa na wajibu ambao unapaswa kuutekeleza.

Kwa bahati mbaya sana hakuna anayeweza kukuambia wajibu wako ni upi, watu watabahatisha tu kwa namna wanavyokuona wewe, lakini hawawezi kupatia.

Ni Carl Jung aliyewahi kusema dunia huwa inakuuliza wewe ni nani, na kama huna majibu basi inakuambia unapaswa kuwa nani.

Watu wengi wamepangiwa na dunia wawe nani, kitu ambacho kinatofautiana kabisa na kilicho ndani yao na matokeo yake wamekuwa na maisha ambayo hawayafurahii.

Kwenye makala hii ya ushauri tunakwenda kujifunza jinsi ya kujua ndoto sahihi kwako na kuacha kutanga tanga na mengi yanayopita mbele yako.

Kabla hatujaangalia hatua za kuchukua kwenye hili, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Kila nikijitathimini napata mkanganyiko nashindwa kujua Ndoto yangu thabiti ni ipi maana najikuta Kila wakati kadri ninavyo interact na Mambo mbalimbali najikuta natamani kuwa mtaalamu wa Mambo hayo. Mfano 1: Nikiona mziki unavyopigwa natamani kuwa mpiga mziki.
2: Nikisikiliza Sana siasa najikuta natamani kuwa mwanasiasa.
3: Nikiona mtu anaimba najikuta natamani kuwa mwimbaji.
Naomba nisaidie  nawezaje kuijua Ndoto yangu sahihi ni ipi ili nianze kuiishi na kufikia mafanikio. Maana najikuta akili yangu inatanga tanga katika Mambo mengi na kuishia kushindwa katika vyote.” – Gamaliel M.

Alichotushirikishs mwenzetu Gamaliel, ndivyo wengi wanaendesha maisha yao, kutanga tanga na kila aina ya fursa.
Na hadithi za mafanikio ndiyo zimekuwa zinawapotosha watu.
Mtu akisikia mwingine amefuga kuku akafanikiwa, anataka akafuge kuku.
Akisikia mwingine amelima nyanya akafanikiwa anakimbilia kwenye nyanya.
Mtu anahangaika hivyo, muda unakwenda na hakuna hatua anazopiga.

Katika utafiti niliofanya kwa muda mrefu wa namna bora ya kuwasaidia watu kufanikiwa, nimegundua kila anayetaka kufanikiwa anapaswa kujua vitu viwili vikubwa kuhusu yeye.
Kitu cha kwanza ni kujua kusudi la maisha yake, kwa nini yuko hapa duniani.
Kitu cha pili ni kuwa na ndoto kubwa anazozipambania ili kuacha alama hapa duniani.

Nilichogundua pia ni kwamba kama mtu hajajua kusudi la maisha yake, atahangaika na mambo mengi na hataweza kukaa na jambo moja kwa muda mrefu.
Na kama mtu hana ndoto kubwa, ataishi maisha ya kawaida na ya mazoea ambayo hayazalishi matokeo yoyote ya tofauti.

Hivyo kabla ya kujua ndoto yako kubwa, anza na kusudi la maisha yako.
Kulijua kusudi, unapaswa kujisikiliza wewe mwenyewe, maana hakuna mwingine anayejua.
Jisikilize kwa kujiuliza maswali haya na kujipa majibu.

1. Ni vitu gani unapenda sana kufanya kiasi kwamba hujali muda wala ugumu wake?
2. Kama fedha isingekuwa tatizo kwako, yaani kama una fedha ya kutosha kuendesha maisha yako kwa namna unavyotaka, vitu gani ungefanya?
3. Vitu gani wengine wanakusifia sana pale unapovifanya au kuja kwako kukuomba ushauri?
4. Vitu gani huwezi kuvumilia ukiona havifanyiki kwa usahihi. Hata kama haikuhusu unajikuta umeshaingilia na kutaka vifanyike kwa usahihi?
5. Ni watu gani unaowaona ni jukumu lako hapa duniani, maisha yao na changamoto zao unachukulia ndiyo wajibu wako?

Maswali hayo unapaswa kuyajibu kutoka ndani ya nafsi yako na hapo ndipo utaweza kujua kusudi la maisha yako, uko hapa duniani kufanya nini.

Ukishalijua kusudi, sasa unaweza kuweka ndoto kubwa unazotaka kufikia.
Kwenye kuweka ndoto, angalia ni matokeo gani makubwa unayotaka kuzalisha au kufikia kwenye maisha yako. Hapa usiangalie njia kwanza, bali angalia matokeo unayotaka kufikia.
Kuwa na picha kabisa kwenye fikra zako, picha inayoonesha ukiwa umefika kwenye ndoto zako na kuamini ni kitu halisi kabisa kwako.

Ukishaweka ndoto zako kubwa, sasa unakwenda kuweka malengo ya kufikia ndoto hizo.
Kusudi na ndoto havipaswi kubadilika sana na mara kwa mara. Ila malengo yanaweza kubadilika kadiri unavyokwenda.
Unachotaka ni kuishi kusudi lako na kufikia ndoto zako kubwa.
Malengo unayofanyia kazi kila siku ndiyo njia. Unapaswa kujifanyia tathmini ili kuona kama utafika kwenye ndoto na kuishi kusudi au la.
Kama malengo hayakufikishi kwenye ndoto, unapaswa kuyabadili.

Ni ruhusa kutanga tanga kwa muda.
Kama hujajua kusudi na ndoto zako, ni ruhusa kutangatanga kwa muda.
Lakini usitange tange kwa matamanio tu, bali fanya majaribio.
Kama umeona wanamuziki na ukaona unapenda kuwa mwanamuziki, tunga wimbo, nenda karekodi kisha sambaza kwa watu wengi. Ona kama mchakato mzima wa kutunga, kurekodi na kusambaza unaweza kuuvumilia.

Kama umeangalia wanasiasa na kuona unatamani kuwa mwanasiasa, ingia kwenye siasa, tafuta uchaguzi wowote na ingia ugombee, au angalia kampeni zozote zinazoendelea na jiunge nazo. Au anzisha kampeni kwenye jambo fulani, kisha pambana na hilo na uone kama ni kitu unaweza kuvumilia kufanya.

Chochote unachovutiwa kufanya, kifanyie jaribio la kuingia moja kwa moja ili uone nini kipo ndani.
Mara nyingi unaweza kutamani vitu kwa nje, ila unapoingia ndani ndiyo unaona vitu ambavyo awali hukuona.
Unapoingia na kufanya, unajua kweli kama ni kitu upo tayari kukipambania au ulikuwa tu na matamanio ya nje.

Usitangetange milele.
Kwenye makala ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu niliandika kujua kusudi lako sema ndiyo, kuliishi sema hapana.
Huwezi kuendesha maisha yako kwa kutangatanga na kila aina ya majaribio.
Hivyo jipe kipindi cha kujaribu vitu mbalimbali, huku ukiangalia kipi kinaendana na wewe.
Ukishapata kinachoendana na wewe, weka nguvu zako kwenye hicho na achana na vingine vyote.

Kila mmoja wetu anaweza kulijua kusudi lake na kuwa na ndoto kubwa kama ataacha kukimbizana na dunia na akajisikiliza yeye mwenyewe.
Hapa umepata mchakato wa jinsi ya kujisikiliza ili ujue kusudi na kuweka ndoto zako kubwa, fanyia kazi mchakato huu ili uweze kuishi maisha yanayoacha alama hapa duniani.

Kama unapenda usimamizi wa karibu katika kulijua kusudi na kuwa na ndoto kubwa unazoziishi, karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA.  Kwenye KISIMA nafanya kazi na mtu mmoja mmoja kuhakikisha anajua kusudi lake na anapambana kuishi ndoto kubwa.
Hii ni fursa ambayo huwezi kuipata sehemu nyingine yoyote, hivyo kama bado hujawa mwanachama, karibu sasa. Tuma ujumbe kwa wasap namba 0717 396 253 kupata maelezo zaidi.

Fanyia kazi haya uliyojifunza kwenye hii makala ili uweze kujua kusudi la maisha yako na ndoto sahihi kwako kuzipigania.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.