2362; Fursa zilizo ndani ya changamoto…

Tunaposema kila changamoto ina fursa ndani yake, siyo ru kujifurahisha kwa kuwa chanya, bali ndiyo uhalisia.

Hata kama linalokukabili ni kubwa na baya kiasi gani, bado kuna mazuri mengi ndani yake ambayo unaweza kuyafanyia kazi.

Kama huzioni fursa zilizo kwenye changamoto, siyo kwa sababu hazipo, bali kwa sababu hujazitafuta.

Kumbuka tunapata kile tunachotafuta, ukiangalia matatizo utayaona hayo kila mahali na ukiziangalia fursa pia utaziona kila mahali.

Leo nakushirikisha mwongozo wa kuziona fursa kwenye kila changamoto au tatizo.

  1. Anza kwa kujiuliza ni kwa namna gani changamoto hiyo inaleta ukuaji binafsi kwako. Hapa kumbuka kauli ya Nietzche kwamba kisichokuua kinakuimarisha. Chochote unachokabiliana nacho, kinapaswa kukuacha ukiwa imara kuliko ulivyokuwa awali.

  2. Angalia upande wa fedha, kama changamoto inataka uwe na fedha zaidi basi itumie hiyo kama sababu ya kukusukuma kupata fedha zaidi. Labda awali ulikuwa huweki uzito sana kwenye kupambana kuongeza kipato chako, uliridhika na ulichokuwa nacho. Sasa mambo yamebadilika na unalazimika kujituma zaidi.

  3. Angalia upande wa muda, ni kwa namna gani changamoto inakupa muda zaidi au inakusukuma ujali muda wako zaidi. Kama changamoto imefanya uwe na mengi ya kufanya, hapo lazima upangilie vipaumbele vyako upya, upunguze mengi yasiyokuwa muhimu.

  4. Upande wa mahusiano pia ni wa kuangalia, ili uone jinsi changamoto inavyokusukuma kuboresha mahusiano yako na wale wa karibu kwako.

  5. Bila kusahau upande wa kujifunza na kujaribu vitu vipya, kupitia changamoto hiyo au fursa unazoziona ndani ya changamoto.

Haijalishi umekutana na changamoto gani, kama bado upo hai kwanza shukuru, kisha jiulize ni manufaa gani yaliyo ndani ya changamoto hiyo.
Fungua macho, masikio na akili yako, orodhesha kila wazo unalopata na chagua yale unayoweza kufanyia kazi.

Kila changamoto ina fursa ndani yake, usisahau hili.

Kocha.