2378; Maamuzi Mapya Kulingana Na Taarifa Mpya…
Watu huwa hawapendi kukubali kama wamekosea.
Hivyo watu wakishaonesha msimamo fulani, wataendelea na msimamo huo hata kama utawaonesha ushahidi mkubwa kwamba hawako sahihi.
Hii ndiyo maana ubishani huwa hausaidii, kwa sababu kadiri unavyombishia mtu, ndivyo unazidi kumfanya asimamie upande wake. Maana alikubaliana na wewe maana yake anakiri kwamba alikosea, kitu ambacho hayupo tayari kufanya.
Pale unapohitaji sana watu wabadili maamuzi yao, epuka kuwaonyesha kwamba walikosea na badala yake waonyeshe kuna taarifa walikuwa hawajapata.
Badala ya kuwaambia umekosea hapa, unawaambia kuna taarifa hii ulikuwa hujaipata bado.
Mtu anapoona kuna taarifa mpya anapata, anakuwa tayari kufanya maamuzi mapya, ambayo ni tofauti na yale ya awali.
Mfano mzuri ni kwenye mauzo, chochote unachomshawishi mtu anunue, atakuja na mapingamizi.
Sasa badala ya kupangua mapingamizi hayo na kumwonyesha mteja kwamba anakosea, unapaswa kutafuta taarifa mpya utakazompa, zitamazomfanya aweze kubadili maamuzi yake.
Mara zote kuwa na akiba ya vitu vipya unavyoweza kumshirikisha mtu, ili apate maarifa ya kutumia kama sababu ya kubadili msimamo wake.
Usitengemee kuwa tu king’ang’anizi na msumbufu ukitegemea mtu atachoka na kukubaliana na wewe.
Hakuna anayependa kukiri amekosea, ila kila mtu anapenda kuonekana anaelewa mambo vizuri.
Tumia hilo la uelewa kuweza kuwashawishi watu wabadilike, kwa kuona wamepata maarifa mapya na kuelewa zaidi kile ambacho hawakuwa wameelewa.
Kocha.