Rafiki yangu mpendwa,
Changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ni zawadi kubwa sana kwetu.
Kwani hizo ndizo zinatupa nafasi ya kujitofautisha na wengine na kupiga hatua zaidi.
Na kwa kuwa wengi wanaokutana na changamoto hizo wanakata tamaa, wewe ukiweza kizivuka unafanikiwa sana.

Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
Hapa tunakwenda kujifunza jinsi ya kuingiza kipato kupitia uandishi.
Msomaji mwenzetu aliyetuandikia akiomba ushauri kwenye hili alikuwa na haya ya kusema;

“Mimi ni Mwalimu na Mwandishi Naandika Makala ya Kuelimisha Na Kufundisha Watu mtandaoni Changamoto yangu ni kwamba Nashindwa Namna Ya Kuanza Ili Makala Ninazoandika ziweze kuniletea Faida(kipato) Ahsante.” – Joshua E. G.

Mtandao wa intaneti umerahisisha sana uandishi na kuwafikia walengwa.
Kabla ya mtandao wa intaneti, ili uwe mwandishi ilibidi kwanza uandike pendekezo, lipitiwe na wahariri, walikubali ndiyo upewe nafasi ya kuchapa kazi zako na ziwafikie wengi.

Mtandao wa intaneti umeondoa kabisa kikwazo hicho cha kusubiri mpaka ukubaliwe na watu. Sasa hivi mtu mwenye ujumbe wowote ule anaweza kuwafikia wasomaji moja kwa moja bila ya kusubiri upewe ruhusa na yeyote yule.

Uhuru huu mkubwa umekuja na changamoto zake, kwa sababu kila mtu anaweza kuwa mwandishi, basi wengi wanafanya hivyo. Kinachotokea ni ushindani kuwa mkali na fursa ya kutengeneza kipato kuwa ndogo.

Pamoja na changamoto hizo, bado kuna fursa kubwa za mtu yeyote kuweza kutengeneza kipato kwa uandishi kupitia mtandao wa intaneti.
Hapa tunakwenda kujifunza mambo ya kuzingatia ili uweze kutengeneza kipato kwa uandishi.

I. Namba muhimu za kuzingatia.
Eneo la kwanza kuzingatia ili kuingiza kipato kupitia uandishi ni namba. Kuna namba muhimu sana unazopaswa kuzijua na kuzifanyia kazi ili uweze kufikia lengo hilo.
Hapa tutaangalia namba mbili muhimu unazopaswa kufanyia kazi.

Moja; theluthi tatu.
Katika uandishi wako kwa wale unaowalenga, watagawanyika kwenye theluthi tatu.

Theluthi ya kwanza ni wale watakaokubaliana na kile unachoandika. Hawa ndiyo utakaowapenda na kutamani watu wote wawe hivyo, kitu ambacho hakiwezekani.

Theluthi ya pili ni wale watakaopinga kile unachoandika, watakikataa wazi wazi na kukupinga au kukukosoa kwa namna ya kukukatisha tamaa. Hawa hutawapenda na utatamani wasiwe wengi.

Theluthi ya tatu ni wale wasiojali, ambao hawajui hata kama unaandika. Hawa hawakufuatilii kwa namna yoyote ile hivyo hawajui wala hawajali unachofanya.

Ni muhimu kujua theluthi hizi tatu, ili uweze kufanyia kazi theluthi moja ya wanaoelewa kile unachofanya na kuachana na hizo theluthi nyingine.

Unapoanza uandishi, unakuwa humuelewi mtu ambaye hakubaliani na kile unachoandika. Unamuona ni kama mtu aliyepotoka na kutamani umlazimishe akuelewe. Ukizijua hizi theluthi utajipunguzia makwazo yanayotokana na wale unaokutana nao.

Mbili; moja ya kumi ya moja ya kumi.
Kwa ile theluthi moja ya watu wanaoelewa na kukubaliana na unachoandika, nayo imegawanyika kwenye makundi mawili.

Kundi la la kwanza ni moja ya kumi ya hiyo theluthi moja, hawa ndiyo watakuwa wasomaji wa mara kwa mara wa kazi zako. Hawa watakufuatilia kwa karibu na ukipita muda hujaandika watakuuliza vipi mbona siku hizi hatupati maatifa yako.
Wengine watakuwa wasomaji, lakini siyo wa mara kwa mara, wakipata nafasi wanasoma, wakikosa hawasomi, ukipote hawakuulizii.
Hivyo moja ya kumi ya theluthi ya wanaokukubali watakuwa wasomaji wa mara kwa mara.

Kundi la pili ni moja ya kumi ya wasomaji wa mara kwa mara ndiyo watakuwa walipaji kwenye uandishi wako. Kwenye wale wasomaji wa mara kwa mara ulionao, ni moja ya kumi ambao watakuwa tayari kukulipa kwenye uandishi wako. Hawa ndiyo watakaokuwa tayari kulipia bidhaa na huduma zako mbalimbali za uandishi.

Kwa kujua namba hizi, ni rahisi kwako kuweka malengo na kuyafanyia kazi.
Mfano kama unataka uwe na wasomaji 100 walio tayari kulipia, inabidi uwe na angalau wasomaji wa mara kwa mara 1,000 na wasomaji wa jumla, wanaoelewa na kukubaliana na unachoandika 10,000.

Kokotoa namba zako na pambana kuzifikia, utayaona matokeo mazuri.

II. Bure yenye thamani kubwa.
Unapoanza uandishi, hakuna wanaokujua na kukuaminini kwenye kile unachofanya.
Hivyo unahitaji kuweka kazi kubwa kwenye kujenga jina lako na kutengeneza wafuasi wanaokuamini na kuwa tayari kukulipa.
Unapofanya uandishi na kutaka kulipwa ndiyo unagundua hakuna kitu kigumu duniani kama kumshawishi mtu akupe fedha zake. Kwa sababu amezipata kwa uchungu na ana matumizi mengi na fedha hizo.
Hivyo lazima mtu aamini anakwenda kupata thamani kubwa sana kwa kukupa fedha zake.
Kujenga hilo, unapaswa kuanza kwa kuwapa watu thamani kubwa mno kwa bure kabisa. Yaani wape watu maarifa ya bure ambayo wao wenyewe hawaamini kama wanayapata bure.
Wafanye watu waone kama wanakuibia hivi, maana kwako wanapata bure kile ambacho wakienda pengine wanatozwa fedha.
Ukijijenga kwa namna hii, unapokuja kuwataka watu walipie hawatakuwa na wasiwasi, maana walishapata thamani kubwa kwako bure hivyo wanaona hata wakilipia hakuna watakachopoteza.
Chochote unachowashirikisha watu hakikisha kuna hatua ambazo mtu anaweza kuchukua na akayaona matokeo mazuri, kwa maisha yake kuwa bora zaidi. Matokeo mazuri ambayo watu wanayapata kupitia kazi zako ndiyo yanawafanya wakuamini zaidi.

III. Jipe muda.
Kama unaingia kwenye uandishi ukidhani ni njia ya mkato ya kupata fedha haraka na bila ya kuweka kazi unajidanganya.
Kama unafikiri ukishakuwa na kitabu basi watu watakimbilia kukinunua kwa sababu ni kizuri sana na wanakihitaji mno pia unajidanganya.
Kutengeneza fedha kupitia uandishi ni kitu kinachowezekana, ila kinahitaji mambo makubwa mawili; kazi na muda.
Lazima uweke kazi kubwa kwenye kusoma na kufanya tafiti ili kuja na maarifa bora yanayoweza kuwasaidia watu.
Lazima pia ujipe muda wa kutoa thamani na kukuza namba zako ili zifikie kiwango ambacho unaweza kuingiza kipato kizuri.
Kama unataka kufanya uandishi kama kitu cha kujisikia tu, hutaweza kuingiza kipato unachotarajia.
Uandishi ni kazi kamili, inayohitaji juhudi kubwa ili uweze kufanikiwa.

IV. Vitabu.
Hatua ya kwanza ya watu kuanza kukulipa kupitia uandishi ni kwa vitabu.
Kadiri unavyoendelea kuandika, kuna vitu watu watakuwa wanakuuliza sana au kukuomba ushauri.
Kusanya yale unayoulizwa sana kisha andika kitabu kinachojibu kwa kina na kumpa mtu suluhisho na hatua za kuchukua.
Hii ndiyo inakuwa bidhaa yako ya kwanza na ambayo pia itakuwa rahisi kwako kuuza.
Maana watu wanapokuuliza au kukuomba ushauri, unawaelekeza wanunue kitabu chako ambacho kina majibu yote muhimu.
Uzuri wa vitabu unaweza kuanza kutoa kwa nakala tete, yaani hukichapi ma hivyo kunakuwa hakuna gharama za uzalishaji.
Lakini pia kitabu ukishaandika mara moja unaweza kuuza kwa muda mrefu, bila kuingia muda au gharama za ziada.
Ni wewe kuendelea kukuza namba zako na wapya wanaokuja kwako kuwashawishi kununua vitabu vyako, hasa baada ya kuwapa thamani kubwa bure.

V. Kozi/uanachama.
Vitabu ni bidhaa ya kwanza, ambayo utauza kwa bei rahisi japo umeweka thamani kubwa.
Vitabu huwa havina faida kubwa kwenye uandishi, hasa pale soko lako linapokuwa dogo.
Hivyo unapaswa kutumia vitabu siyo kama biashara yako kuu, bali njia ya kuendelea kuwashawishi wasomaji wako wapate huduma zaidi kutoka kwako.
Hatua ya pili ya kukipwa kupitia uandishi ni kuwa na mafunzo unayoyatoa kupitia kozi au mfumo wa uanachama.
Hapa mtu analipa ada ili kupata mafunzo zaidi kutoka kwako.
Hatua hii unaweza kutengeneza faida nzuri kwani ada utakayotoza ni kubwa ukilinganisha na vitabu na kama ukiwa na namba nzuri ya wasomaji, kipato kinakuwa kizuri.
Uzuri wa kozi ni kwamba unaweza kuandaa mara moja na watu wakaendelea kujifunza kadiri wanavyokuja wapya.
Pia kwa mfumo wa wanachama, unaweza kuwa na masomo mengi ambayo watu wanayafuatilia na hata wapya wanaokuja wanapata na ya nyuma pia.

VI. Ushauri/usimamizi.
Hatua ya juu kwenye kuingiza kipato kupitia uandishi ni ushauri au usimamizi kwa wale wanaotaka kupiga hatua zaidi.
Hapa mtu anakuwa amedhamiria kweli na yupo tayari kuwekeza ili apate matokeo makubwa.
Kwa kuwa huwezi kufanya kazi na kila mtu, lazima ada unayotoza kwenye huduma hii iwe kubwa, ili ifidie muda na uzoefu wako, lakini pia ikusukume kutoa thamani kubwa zaidi.

Mchakato huu unahitaji juhudi kubwa, muda na uvumilivu pia. Mambo hayatakwenda kirahisi na kwa mtiririko mzuri kama nilivyoelezea hapa, kuna magumu na changamoto utakazokutana nazo. Muhimu ni uendelee kuweka juhudi na usikate tamaa.

Kwa uhitaji wa kusimamiwa kwa karibu ili uweze kujijenga kiuandishi na kuingiza kipato kupitia uandishi wako, tuwasiliane kwa wasap namba 0717 396 253.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.