2379; Wateja Bora Wa Biashara Yako…

Wateja bora kabisa wa biashara yako ni wateja ambao walishanunua kwako na wakapata kile walichotegemea kupata.

Hawa ni rahisi kuwashawishi wanunue tena kuliko kuwashawishi wateja ambao hawajawahi kununua kabisa.

Hivyo unapofanya biashara yoyote ile zingatia vitu hivi vitatu muhimu na ambavyo vitaiwezesha biashara kufanikiwa sana.

Kitu cha kwanza ni kufanya mteja kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye biashara. Kwanza kwa kutoa thamani kubwa kabisa ambayo mteja hawezi kuipata kwingine na kuhakikisha unampa mteja kile ambacho kina manufaa kwake.

Kitu cha pili ni kuhakikisha humpotezi mteja ambaye alishawahi kununua kwako. Huyu endelea kumfanya abaki kwenye biashara. Endelea kuwasiliana naye, endelea kujua mahitaji yake na endelea kupambana kuyafikia. Usikubali kupoteza mteja ambaye alishawahi kununua kwako, hata kama hana mahitaji tena, endelea kumweka kwenye mawasiliano, kuna wakati atakuwa na manufaa kwako.

Kitu cha tatu, pale mambo yanapokuwa magumu kibiashara, fanya kitu kipya kwa wateja wa zamani. Kwa kuwa tayari unao wateja wa zamani, ambao ni kama mgodi wa dhahabu kwako, unapaswa kuutumia kama njia ya kujiokoa pale mambo yanapokuwa magumu. Hapa unahitaji kuangalia wateja wa zamani ulionao na kujua kipi wanahitaji zaidi na kuwapatia, hilo litakuondoa kwenye ugumu wowote unaoweza kuwa unapitia. Katika kutekeleza hili, kumbuka namba moja.

Tayari biashara yako ina wateja bora, ni wewe kuwatumia vizuri na kuendelea kutengeneza wengine bora pia. Mteja akishanunua, mfanye kuwa sehemu ya familia ya biashara yako.

Kocha.