2382; Usiige anasa zisizo saizi yako…

Kama bado hujafikia uhuru wa kifedha, anasa yako ni moja tu, kazi.
Usidanganyike na mlinganyo wa maisha na kazi.
Usidanganyike na kufanya kazi kwa akili na siyo kwa nguvu.
Hizo ni anasa za wale ambao tayari ‘wametoboa’.

Kwako wewe huhitaji mlinganyo wa maisha na kazi, maana maisha yako na kazi ni kitu kimoja. Kazi ndiyo maisha yako.
Huhitaji kupoteza muda kujiuliza kama unafanya kwa nguvu au kwa akili. Unafanya kwa vyote, nguvu na akili.

Wote unaowaona wameshindwa sasa, kuna maamuzi waliyafanya huko nyuma, ambayo yalitoa vipaumbele kwa mambo mengine tofauti na mafanikio waliyokuwa wanayataka.

Hata ulipo wewe sasa ni matokeo ya maamuzi na vipaumbele ulivyojipa huko nyuma.
Kutoka hapo, lazima ufanya maamuzi na vipaumbele vya tofauti.

Wanasema ujinga ni kufanya kitu kile kile, kwa namna ile ile halafu kutegemea matokeo ya tofauti.
Jiulize kazi uliyonayo umeifanya kwa miaka mingapi sasa na sasa unaifanyaje tofauti na kipindi cha nyuma?
Kadhalika kwa biashara, jiulize umeifanya kwa miaka mingapi sasa na ni namna gani unaifanya kwa utofauti sasa?

Unaweza kujiona unaweka juhudi na kujituma sana, lakini matokeo unayoyapata yasiwe makubwa, sababu inakuwa ni namna ulivyoweka vipaumbele vyako.

Kama una kipaumbele kingine kinachozidi kazi au biashara yako, jua hicho kitashindana na kazi au biashara na kitashinda.
Kama una kipaumbele kingine muhimu zaidi ya kufikia uhuru wa kifedha, utapata kipaumbele hicho ila utakosa uhuru wa kifedha.

Waliofanikiwa sana hupewa majina mabaya. Huonekana ni watu wabaya na wasiojali, wenye tamaa na wanaowanyonya wengine.
Lakini yote hayo ni kwa sababu watu hao wameweka vipaumbele vyao na hawapo tayari kuvivunja kwa namna yoyote ile.

Kama wamejiambia wanataka kufika mahali fulani, watafika hapo na hawatamhurumia yeyote atakayekuwa kikwazo kwao kufika wanakotaka kufika.

Unahitaji kuweka upya vipaumbe vyako ili uwe na moto sahihi wa kukusukuma kufika kwenye mafanikio makubwa.

Kocha.