2383; Furahia Kupitwa…

Mitandao ya kijamii imekuwa inakunasa kwenye uraibu kwa kukufanya uone kama unapitwa.

Sisi binadamu tunahofia sana kupitwa na yale muhimu, maana kutokupitwa ndiyo kuliwawezesha watangulizi wetu kuepuka hatari mbalimbali na kuweza kuendeleza kizazi cha binadamu hapa duniani.

Kipindi cha nyuma ilikuwa hatari sana kwa mtu kukaa na kufanya mambo kwa peke yake, maana kuna mengi ambayo mtu hakuweza kujua.

Kuwa ndani ya kundi la jamii ilikuwa njia salama ya kuepuka hatari hizo. Na unapokuwa kwenye kundi hilo unahakikisha unajua kila kinachoendelea, hupitwi na chochote.

Zama zimebadilika, zile hatari hazipo tena ila mazoea bado yapo. Bado tunasukumwa kutaka kujua kila kinachoendelea, hasa kwenye mitandao ya kijamii kwa hofu kwamba tukipitwa ni hatari.

Ili uweze kupata muda na umakini kwenye zama hizi, lazima uwe tayari kuigeuza hofu ya kupitwa (FOMO – fear of missing out) kuwa raha ya kupitwa (JOMO – joy of missing out).

Yaani furahia kabisa kupitwa, ukijua hakuna lolote la maana linalokupita hasa kwenye nitandao ya kijamii.
Jua kabisa kwamba muda unaookoa na kuutunia kwa yale muhimu una manufaa zaidi.

Kila unapoingiwa na hofu ya kupitwa, jikumbushe jinsi ilivyo raha kupata muda na umakini wa kuweka kwenye vitu muhimu zaidi.
Hilo linabadili kabisa mtazamo wako kitu kinachokupa utulivu mkubwa.

Hakuna cha maana kinachokupita mtandaoni, furahia kupitwa kwa sababu unapata muda na umakini wa kufanya yale muhimu zaidi.

Kocha.