2384; Sababu na visingizio…

Kuna vitu huwa unapanga au kupenda kufanya, lakini unashindwa kukamilisha kama ulivyopanga.

Huwa unatoa sababu mbalimbali kwa nini umeshindwa kufanya au kupata unachotaka.
Lakini kiukweli kabisa nyingi unazotoa siyo sababu, bali ni visingizio.

Sababu ni vile vikwazo au changamoto za kweli kabisa, ambazo zinamzuia kila mtu.

Visingizio ni kitu unachotumia kuficha uzembe na uvivu wako. Kwani wewe unakuwa umezuiwa, wakati kuna wengine wamevuka hilo.

Hivyo unapaswa kuacha kutumia visingizio kama sababu, jiambie wazi unajipa visingizio ili uache kujidanganya.

Kama kitu kwako ni kikwazo au changamoto, lakini wengine wameweza kukivuka, hiyo siyo sababu bali ni kisingizio.

Kama unasema umeshindwa kuanza biashara kwa sababu huna mtaji, wakati huo kuna watu wameanzisha biashara bila kuwa na mtaji, hiyo siyo sababu, ni kisingizio.

Kama unasema huwezi kuanzisha biashara ukiwa kwenye ajira, wakati wapo walioweza kufanya hivyo, hicho ni kisingizio.

Anza kupitia sababu zote unazojipa kama kikwazo kwako kufanikiwa, angalia kama kuna wengine wameweza kufanikiwa licha ya kuwa na vikwazo hivyo, kama wapo jua hiyo siyo sababu, bali ni kisingizio.

Na unapojitafakari kwa nini hujafanikiwa, acha kujiambia kwa sababu, jiambie kwa kisingizio…..
Kwa kuwa wazi kwako mwenyewe, utaziona hatua sahihi kwako kuchukua ili kufanikiwa.

Kocha.