Rafiki yangu mpendwa,
Kauli huwa zinaumba.

Kauli zinaumba kwa sababu zinatokana na mtazamo na imani zilizo ndani yetu.

Kauli tunazotumia zinatokana na kile tunachoamini.
Unaweza kujiambia ni kauli ya kawaida tu, ila kama unaitumia, jua ina nguvu kubwa sana kwako.

Kuna kauli kumi ambazo kama unazitumia kamwe huwezi kufanikiwa.  Kauli hizo zinakuwa kiashiria cha mtazamo na imani ulizonazo.

Zifuatazo ni kauli kumi ambazo zinaashiria huwezi kufanikiwa. Kama umekuwa unazitumia, unapaswa kuchukua hatua za makusudi za kubadili kabisa mtazamo wako ndiyo uweze kufanikiwa.

1. Pesa hainunui furaha.
Hii ni kauli maarufu sana kwa walio masikini. Ukisikia mtu anatumia kauli hii jua kwa uhakika ni masikini na hawezi kuwa tajiri.
Matajiri wa kweli hawazungumzii fedha kuhusiana na furaha, wanajua jinsi gani fedha inaweza kununua furaha wanayoitaka.
Kama umekua unatumia kauli hii, achana nayo mara moja na elekeza nguvu zako kwenye kupata fedha za kutosha kwanza, halafu utaona jinsi unavyoweza kuzitumia kununua furaha.

2. Kama ipo ipo tu.
Hii ni kauli inayopenda kutumiwa na wavivu na wazembe ambao hawapo tayari kujituma. Waumini wa kauli hii huwa wana mtazamo mgando, wakiamini kama ni mafanikio mtu amepewa au hajapewa, juhudi ambazo mtu anaweka haziwezi kubadili hatima yake.
Hii siyo kweli, juhudi ambazo mtu anaweka zina nguvu ya kubadili hatima yake. Hivyo usiamini kama ipo ipo tu, bali jua kama ikiwekewa juhudi inapatikana.
Amini sana kwenye juhudi badala ya hatima, kuwa na mtazamo wa ukuaji badala ya mtazamo mgando.

3. Hatuwezi wote kuwa matajiri.
Kauli nyingine inayopendwa na masikini ni hii kwamba watu wote hatuwezi kuwa matajiri. Na hilo ni kweli kabisa, kwani hata kwenye nchi tajiri duniani, bado masikini wapo.
Na sababu kubwa ni kwamba umasikini ni hali ya kifikra na kimtazamo zaidi. Kwani hata pale masikini hao wanapopewa fedha, huishia kuzipoteza zote.
Sawa, tumekubali kwamba wote hatuwezi kuwa matajiri, lakini kwa nini wewe uchague kuwa sehemu ya masikini?
Kama kuna wachache watakaokuwa matajiri, kwa nini wewe usiwe mmoja wao?
Kama wao wanaweza, nini kinakushinda wewe?
Usijitolee kuwa masikini kama vile ndiyo utakatifu, chagua kuwa kati ya matajiri wachache na weka juhudi kufikia hilo.

4. Kila mtu akijiajiri nani atamuajiri mwenzake.
Kauli inayopenda kutolewa sana na wale ambao hawana uthubutu wa kwenda kufanyia kazi ndoto zao.
Watu hao huwa wanakuwa na ndoto zao kubwa, ila hawana uthubutu wa kuzifanyia kazi.
Lakini hawataki kukiri kwamba wanachokosa ni uthubutu, hivyo wanatafuta sababu nyingine kama hiyo ya kila mtu akijiajiri nani atafanya kazi za kuajiriwa zilipo.
Na kama nilivyoeleza kwenye utajiri hapo juu, kwa nini uchague mwenyewe kwenda kundi lisilo sahihi?
Ndiyo kuna watu lazima waajiriwe na kutumikishwa, lakini siyo lazima wewe uwe mmoja wao au uwe hivyo milele.
Una nguvu ya kuchagua chochote unachotaka kama utabadili mtazamo wako na kuwa na uthubutu wa kufanya ya tofauti.

5. Sina bahati  nzuri.
Mtu mmoja aliyefanikiwa aliwahi kuambiwa ana bahati sana. Akajibu ni kweli nina bahati, na kadiri ninavyoweka juhudi zaidi, ndivyo ninavyopata bahati zaidi.
Bahati siyo kitu kinachotokea tu, bahati ni kitu kinachotengenezwa, kwa kutumia juhudi ambazo mtu anaweka.
Bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa nzuri.
Hivyo usiseme huna bahati, bali sema unatengeneza bahati.
Una nguvu ya kutengeneza bahati yoyote unayotaka, unachohitaji ni kuweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya na kukifanya kwa utofauti mkubwa na wengine wanavyofanya.

6. Mimi ni mnyonge.
Hata vitabu vya dini vinaeleza wazi, hakuna kinyonge kitakachouona ufalme wa mbinguni.
Hivyo kama unatumia kauli hii kwamba wewe ni mnyonge, jua huwezi kufanikiwa kamwe.
Wanasiasa wanapenda kukuaminisha kauli hiyo, kukuambia kwamba lengo lao ni kukukomboa wewe mnyonge. Lakini lengo lao ni kuendelea kukufanya uwe tegemezi kwao.
Kataa kabisa unyonge, kama uko hai na una afya njema, wewe siyo mnyonge, una uwezo mkubwa wa kuyajenga maisha yako kwa namna unavyotaka.
Kataa unyonge, shika hatamu ya maisha yako na fanya makubwa.

7. Maisha ni haya haya.
Kauli inayopenda kutumiwa na wale ambao wanayapoteza maisha kwa kufanya vitu vya hovyo, wakiamini hakuna maisha mengine.
Watu hawa hupoteza muda na maisha yao na hawaachi alama yoyote hapa dubiani.
Watu wote waliofanya makubwa hapa duniani, wamekuwa wakiendelea kuishi hata baada ya kufa. Majina yao hayafutiki.
Hivyo acha kupoteza muda na maisha yako ukiamini maisha ni haya haya tu na inabidi uyaishi kwa raha na anasa muda wote.
Yatoe maisha yako kwa ajili ya kitu kikubwa, kitu kitakachofanya jina lako liendelee kuishi hata baada ya kufa kwako.

8. Kila mtu atakufa.
Kauli inayotumiwa sana na wale ambao hawataki kuweka malengo ya miaka mingi ijayo.
Muulize mtu unajiona wapi miaka 10 ijayo, atakuambia ya nini kujisumbua na yajayo?
Muulize mtu anakiona wapi kile anachofanya miaka 50 ijayo na atakushangaa tu.
Haishangazi kwa nini baadhi ya watu wanaweza kupambana na kujenga mafanikio, ila wanapokufa na mafanikio yao yanakufa.
Ni kwa sababu wanakosa mipango ya muda mrefu.
Wewe usifanye kosa hili, kuwa na malengo na mipango ya muda mfupi na muda mrefu.
Jua unataka kufika wapi mwaka mmoja ujao, miaka mitano, 10 na hata 20 ijayo.
Kile unachofanya kuwa na ndoto za miaka 100 ijayo, ndiyo hautakuwepo lakini jua kitaendelezwaje wakati ambao hutakuwepo.
Usikubali kutumia maisha yako kujenga kitu ambacho kitakufa kwa haraka pale unapoondoka, jenga misingi ambapo kitu kitadumu kwa muda mrefu hata baada ya kuondoka kwako.

9. Matajiri wana roho mbaya.
Kinachowafanya masikini wengi kuzidi kubaki kwenye umasikini ni kuwachukia matajiri na utajiri. Ukishakichukia kitu, akili yako haiwezi kukuruhusu uwe nacho, maana inakukinga na yote mabaya kwako.
Badili mtazamo wako kuhusu utajiri na matajiri.
Amini utajiri ni kitu kizuri na matajiri ni watu wazuri, kitu ambacho ni kweli kwa sababu wana mchango mkubwa kwenye uchumi.
Ukipenda utajiri na matajiri, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya wewe pia kupata utajiri.
Kaa mbali na wale wanaoponda utajiri na matajiri, sumu yao ni kali.

10. Tayari najua hayo, sina haja ya kuyasoma.
Wabishi wa kusoma vitabu wanapenda sana kauli hii.
Wao tayari wanajua kila kitu hivyo wanaona hawana umuhimu wa kusoma.
Cha kushangaza ni kama kweli wanajua hayo wanayosema wanajua, kwa nini hawapigi hatua kwenye maisha yao?
Na hapo ndipo unagundua kwamba hiyo ni kauli ya kujifariji na kujidanganya tu.
Kama bado hujafanikiwa, kuna vitu ambavyo bado hujavijua.
Hivyo kuwa tayari kujifunza vitu vipya na kuchukua hatua za tofauti ili uweze kufanikiwa.
Kamwe usijiambie tayari unajua kila kitu, jua kuna mengi hujui, kuwa mnyenyekevu, jifunze, chukua hatua na maisha yako yatakuwa bora.

Ondokana na kauli hizo kumi na nyingine zinazoendana nazo ili uweze kujiondolea ukomo na ufike kwenye mafanikio makubwa.
Ukisoma kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, unajionea wazi jinsi ulivyo na uwezo mkubwa ndani yako.
Hata kama umekuwa unajiona ni wa kawaida na huwezi kufanya makubwa, jua uwezo mkubwa sana umelala ndani yako, ni wewe kuuamsha na kuutumia kufanya makubwa.
Kama bado hujasoma kitabu hicho kipate leo kwa kuwasiliana na 0752 977 170.

Usikubali kuendelea kuwa kikwazo ka mafanikio yako mwenyewe. Badili mtazamo, imani na kauli unazotumia ili vikusukume kufanya makubwa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz