Umewahi kusikia msemo usemo “ukubwa wa utajiri wako unategemea ukubwa wa mtandao wako”. Usemi huu ni wa kweli kabisa ukiufanyia kazi. Kama mtu unayetaka kufanikiwa katika mauzo unapaswa kujenga mtandao mkubwa pia wa watu. Ili iwe rahisi kufanya ufuatiliaji wako.

Zama tulizomo zimetufanya tutegemeane kwa namna moja au nyingine. Hakuna mtu anafanikiwa kwa kufanya mambo kivyake vyake. Hii ni kwa sababu huwezi kujiuzia kila kitu, utahitaji kuwauzia na kununua kwa watu wengine.

Ili ufanikiwe katika mauzo, unapaswa kuweka juhudi za kutosha kwenye kujenga mtandao utakaokuwezesha kufanya mauzo makubwa na kwa muda mrefu.

Maana mauzo sio kitu kinachofanyika siku moja. Ni kitu kinachopaswa kuwa endelevu wakati wote. Ukiwa na mtandao mzuri unakurahisisha kuwafikia watu sahihi na kuwa na ushawishi mkubwa kwao. 

Ni wewe kuweka nguvu kubwa katika kukuza mtandao wako. Pambana sana kutafuta watu wanaofanya kile unachofanya au wameishawahi kufanya hicho unachofanya. Au wanafikiria kufanya hicho kitu. Kupitia mtandao wako unaweza kujifunza kitu kutoka kwao na kukusogeza katika mauzo. 

Maeneo Matano Ya Kujenga Mtandao Wako, Ili iwe rahisi kufanya ni kama;

Moja; Mikutano mbalimbali ya wafanyabiashara.
Hapa unakutana na wengi unaowalenga kwa wakati mmoja na ukitumia vizuri fursa hiyo utaweza kujenga ushawishi kwa wengi.

Mbili; Klabu mbalimbali za kibiashara na kijamii.
Kwenye maeneo mbalimbali huwa kunakuwa na klabu ambazo zinawaleta watu pamoja. Hiyo ni fursa ya kuwafikia wale unaowalenga kama wapo kwenye klabu za aina hiyo.

Tatu; Vikundi vingine vya kibiashara ambavyo huwa vinakutana mara kwa mara. Kila aina ya biashara huwa ina vikundi vyake na mikutano yao, kujua na kuhudhuria itakuwa fursa nzuri kwako.

Nne; Shiriki kwenye kutoa misaada na kujitolea kwenye mambo ya kijamii. Watu wengi wenye uwezo, ambao pia ndiyo unawalenga huwa wanajihusisha na mambo hayo, hivyo ni sehemu nzuri kukutana nao. Fursa nyingi zipo kweye utoaji wa misaada. Sio lazima utoe kitu kikubwa, kidogo tu. Itakusaidia kuonekana mbele ya wengine.

Tano; Maonyesho ya kibiashara.
Huwa kuna maonyesho mbalimbali ya kibiashara ambayo huwa yanafanika. Kwa kushiriki maonyesho hayo unapata fursa ya kuwafikia wengi na walio sahihi kwa wakati mmoja. Mfano Saba Saba na Nane nane. Huko utakutana na watu wengi, wenye mawazo kama yako na itakupa urahisi kuwafuatilia.

Hatua za kuchukua leo; Anza kufuatilia klabu za kibiashara zinazofanyika eneo ulilopo. Pili, tenga fungu dogo, toa msaada kwa wenye huhitaji na kushiriki katika matukio ya kijamii. Ukifanya kwa mwendelezo kuna namna itasaidia wakati wa ufuatiliaji na kukuza mtandao wako. Fanyia kazi yote uliyojifunza katika somo hili.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659.
Mauzo Ni Raha.