3404; Chanjo ya mafanikio.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Chanjo huwa inafanya kazi ya kuchochea na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa fulani.

Kuupa mwili chanjo ni kuufanya upate ugonjwa huo ambao unapaswa kukingwa, lakini unakuwa hauna madhara makubwa
Hivyo mwili unajenga kinga na pale ugonjwa halisi unapokuja, unakosa nguvu ya kuusumbua mwili.

Mwili ambao haujapata chanjo huwa unakuwa dhaifu na kuugua kwa urahisi pale unapopata huo ugonjwa.

Hii dhana ya chanjo inahusikaje kwenye mafanikio?

Tuanze na mifano michache ambayo ni halisi kabisa.

Moja ni watu ambao huwa wanashinda bahati nasibu. Hawa hupata matokeo makubwa ya haraka, lakini huwa hayadumu kwa muda mrefu.

Mbili ni watu ambao wanapata urithi mkubwa. Urithi hubadili kabisa maisha ya mtu. Lakini huwa haichukui muda wanapoteza kila kitu.

Unaweza kuona hapo kuna mwenendo fulani, kwamba mafanikio yanayopatikana kwa haraka huwa yanaishia kwenye upotevu.

Na hapo ndipo dhana ya chanjo ya mafanikio inapoingia.

Kila hatua ambayo mtu unapiga kwenye maisha yako, huwa kuna makosa unayofanya.
Makosa hayo ndiyo yamekuwa yanawapa watu uimara wa kuweza kukabiliana na makubwa zaidi.

Kushindwa ambapo kunamwandaa mtu kupata ushindi mkubwa baadaye ndiyo chanjo ya mafanikio.

Kila makosa unayofanya na kupelekee kushindwa, ni kinga kubwa unayokuwa umejijengea ambayo itakuzuia usichoke wala kukata tamaa pale mambo yanapokuwa magumu.

Unaposhindwa ukiwa kwenye hatua za awali ni kujijengea kinga inayozuia kushindwa kwa ukubwa pale mambo yanapokuwa mazuri.

Kwa makosa unayofanya na kushindwa unakopitia, kunakuwa msingi wako wa kujenga mafanikio makubwa zaidi.
Kushindwa kunakufundishwa kuwa imara,  kuwa tayari kubadilika, na nguvu ya ung’ang’anizi kwenye kujenga mafanikio makubwa.

Pokea kushindwa na magumu unayokutana nayo kwenye safari ya mafanikio kama chanjo inayokupa kinga dhidi ya makubwa zaidi ya baadaye.

Watu hutamani sana kupata ushindi mkubwa bila kukutana na magumu au kutelekeza.
Lakini wanapopata hayo matokeo makubwa na mazuri, tena kwa haraka, huwa wanaishia kupata anguko na kupoteza kila kitu.

Jenga mafanikio yako makubwa hatua kwa hatua, kwa sababu kila hatua inakuimarisha zaidi kadiri unavyozidi kwenda juu.

Lolote unalopitia, ligeuze kuwa rasilimali muhimu ya kufika mbali zaidi ya pale ambapo umefika.
Na hapo utazidi kuwa imara na kuweza kufanya makubwa zaidi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe