2386; Kama bado unajiuliza, jibu ni hapana…

Hakuna siku unaamka asubuhi na kujiuliza kama uko hai au la, kama uko hai unajua uko hai.

Vitu unavyojua kwa hakika kwenye maisha yako huwa hujiulizi ulizi kila wakati, tayari majibu unayo.

Hilo lipeleke kwenye kila eneo la maisha yako, ukiona bado unajiuliza kitu, basi jibu ni bado hujawa na kitu hicho.

Kama bado unajiuliza iwapo umefanikiwa au la, jibu unalo, bado hujafanikiwa. Ukiwa umefanikiwa huwi na haja ya kujiuliza, unajua moja kwa moja.

Kama bado unajiuliza iwapo una furaha au la, jibu ni huna furaha. Ukiwa na furaha huhitaji kujiuliza, jibu unakuwa nalo.

Badala ya kupoteza muda wako kwenye maswali ya aina hiyo, pambana kuchukua hatua sahihi ili upate matokeo ambayo hutahitaji tena kujiuliza maswali hayo.

Kwa maswali yoyote yanayokusumbua, jua hatua unazopaswa kuchukua ili utengeneze majibu ya uhakika, majibu ambayo yatamaliza kabisa maswali hayo.

Unapaswa kuyaishi maisha na siyo kujiandaa kuja kuishi maisha. Kwa maana hiyo, unapaswa kuwa unafanya unachopaswa kufanya na siyo kutamani ungekuwa unafanya kitu fulani.

Ni maswali gani umekuwa unajiuliza sana? Jua hayo ni maeneo ambayo bado hujayajenga vizuri, weka juhudi kwenye kuyajenga.

Kocha.