Rafiki yangu mpendwa,
Najua umewahi kuona misafara ya viongozi wakubwa barabarani.
Misafara hiyo huwa haikai kwenye foleni kama magari mengine.
Badala yake huwa inapewa kipaumbele cha kupita moja kwa moja.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio ya kimaisha.
Walio wengi huwa wanakaa kwenye foleni, ambayo inawachelewesha sana.
Na wachache wanaofanikiwa sana huwa hawakai kwenye foleni, hawa hupita moja kwa moja na kwenda kwenye kile wanachotaka.

Foleni tunazozungumzia kwenye mafanikio siyo ya magari barabarani, bali kufuata utaratibu uliozoeleka kwenye kazi au biashara.

Mtu anayejiambia inadidi asome mpaka ahitimu ndiyo aweze kuanza harakati za maisha yuko kwenye foleni. Anayeingia kwenye harakati za maisha moja kwa moja bila kusubiri mpaka awe na elimu ameruka foleni.

Mtu aliye kwenye ajira na anategemea apande vyeo mpaka kufika ngazi za juu kabisa yuko kwenye foleni. Anayeanzisha biashara yake na kupambana kuikuza ameruka foleni.

Mwandishi anayesubiri mpaka apate au akubalike na wachapaji wakubwa ndiyo atoe kitabu chake yuko kwenye foleni. Mwandishi anayeandika kitabu chake na kukiuza mwenyewe ameruka foleni.

Kwa mifano hiyo michache, unajionea wazi wapi wanaofanikiwa na wanaoshindwa wanatengana. Ukishakubali kukaa tu kwenye foleni, hapo umeagana na mafanikio.

Kukaa kwenye foleni ni kusubiri utaratibu uliozoeleka kwenye kitu fulani. Kukaa kwenye foleni ni kusubiri watu fulani wakupe ruhusa.
Uzuri ni kwamba zama zimebadilika sana kwa sasa, huhitaji kusubiri utaratibu wala ruhusa ya yeyote, unachohitaji ni kujua unachotaka na kukiendea mara moja.

Mwandishi James Altucher kwenye kitabu chake alichokiita Skip the line : the 10,000 experiments rule and other surprising advice for reaching your goals, ametupa mbinu za kuruka foleni na kwenda moja kwa moja kwenye mafanikio yetu.

Najua umeshakutana na njia nyingi za mkato za kufanikiwa, na zote zimekuwa njia za uongo, zilizopoteza muda na fedha zako.
Kuruka foleni siyo njia ya mkato ya kufanikiwa, bali ni njia ya kuacha kusubiri na kupoteza muda kwa yasiyo sahihi na kwenda moja kwa moja kwenye kile unachotaka.

Kupitia kitabu hiki cha SKIP THE LINE, James anatushirikisha sheria ya majaribio 10,000 na ushauri mwingine wa jinsi mtu unavyoweza kufikia malengo yako na kufanya makubwa.
Karibu tujifunze.

UTANGULIZI; RUKA FOLENI.

Kwenye maisha, tangu tukiwa watoto tumefundishwa kukaa kwenye foleni na kusubiri wakati wako ufike ndiyo upate unachotaka.
Unaanza darasa la kwanza mpaka la saba, unaenda kidato cha kwanza mpaka cha nne au sita, unaenda chuo na ukishahitimu ndiyo unakuwa tayari kwa ajili ya kazi.
Ukipata kazi unaanzia ngazi za chini, kisha unasubiri miaka ipite upate uzoefu wa kutosha ndiyo upandishwe cheo na kwenda ngazi za juu.
Ukitaka kupanda cheo zaidi inakubidi urudi tena shule kwenda kuongeza elimu.

Hivyo ndivyo tulivyokuzwa tukiamini na kwa kipindi cha nyuma ilifanya kazi, ka sababu ajira zilikuwepo.
Mtu aliyesoma alikuwa na uhakika wa kupata ajira na akishaipata alikaa nayo mpaka alipostaafu.

Lakini sasa mambo yamebadilika sana, ajira zimekuwa ngumu kupatikana na hata mtu akiipata, hakai nayo muda mrefu. Watu wanabadili kazi mara nyingi katika kipindi cha maisha yao.

Kwenye biashara pia hali ni hiyo hiyo, tulifundishwa kukaa kwenye foleni, kuanzia chini, kukua taratibu mpaka kufika ngazi za juu.
Lakini hali ya biashara kwa sasa ina ushindani mkali ambapo huwezi kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu.

Tatizo ni muda.

Dhana ya kukaa kwenye foleni na kusubiri wakati wako ni nzuri, kwani inamjengea mtu ujuzi na uzoefu mkubwa kabla hajapewa majukumu makubwa.
Lakini tatizo kubwa sana ni muda, hakuna muda wa kutosha kusubiri kwenye foleni.
Nani anaweza kukaa kwenye ajira miaka 10 kusubiri kupandishwa cheo wakati ajira hiyo inaweza kufa muda wowote?

Katika hali ya uchumi tuliyonayo, kusubiri kwenye foleni ni kujichelewesha. Utajizuia usiweze kufikia ndoto zako kubwa.
Katika zama hizi, njia pekee ya kufikia ndoto zako na kupata unachotaka ni kuruka foleni, kutokusubiri mpaka wakati wako ufike, badala yake kutengeneza wakati sahihi kwako.

Watu wengine ni kikwazo.

Wale waliozoea kukaa kwenye foleni na ambao sasa wapo kwenye foleni, hawatakuacha kirahisi uruke foleni.
Chukua mfano wa foleni ya kawaida, labda umeenda benki ukakuta kuna foleni ndefu, halafu wewe ukaona huwezi kusubiri kwenye foleni hiyo, ukaamua kwenda moja kwa mhudumu.
Hawatakuacha ufanye hivyo, watu watapiga kelele, mhudumu atakuambia urudi kwenye foleni yako na ukikataa utaitiwa hata askari akuondoe.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kazi na biashara. Utakapochagua kutokukaa kwenye foleni, utakapoamua kwenda moja kwa moja kwenye kile unachotaka, watu watakuzuia.
Watakuambia huwezi, hujawa tayari, unahangaika sana, una kiherehere na utashindwa.

Kama utawasikiliza watu hao, utaona wako sahihi, kwa kuwa wana uzoefu kuliko wewe na utarudi kwenye foleni.
Lakini pia utakuwa umechagua kutokupata unachotaka.
Njia pekee ya kupata unachotaka ni kuruka foleni na kutokuwasikiliza wale wanaotaka ukae kwenye foleni.

Kuhusu masaa 10,000.

Malcolm Gladwell kwenye kitabu chake cha Outliers alielezea sheria ya masaa 10,000 ambayo iligunduliwa na  Anders Ericsson.
Sheria hiyo inaeleza kwamba ili mtu aweze kufikia ubobezi wa juu kabisa kwenye kile anachofanya, lazima akifanye kwa makusudi kwa masaa yasiyopungua elfu 10.
Kufanya kwa makusudi maana yake ni kujifunza, kufanya huku ukipata mrejesho kutoka kwa kocha anayekufuatilia kwa karibu.
Hivyo ndivyo wachezaji, wanamuziki na hata wavumbuzi wakubwa walivyoweza kufikia ubobezi waliofikia.

Masaa elfu 10 siyo chini ya miaka 10 kama utatenga masaa matatu kila siku bila kuacha hata siku moja.
Lakini kama tulivyoona hapo juu, tatizo ni muda, huna muda wa kutosha kuweka masaa elfu 10 kwenye kitu kimoja.

Kwenye kitabu hiki, James Altucher anatupa mbadala wa masaa elfu kumi ambao ni majaribio elfu kumi.
Katika dhana hii, unajaribu vitu vingi kwenye maisha yako ili kujua kile hasa unachopenda na kisha kukifanya.
Pia unakuwa tayari kubadilika pale hali inapobadilika.

Kama ulisomea taaluma fulani na sasa ajira hakuna au hazilipi vizuri, hujifungii kwenye taaluma hiyo, bali unajaribu vitu vingine mpaka unapata kizuri unachoweza kufanya.
Kadhalika kama umekuwa na biashara na ikafa kutokana na mabadiliko ya uchumi, huoni kama umepoteza kila kitu, bali unakuwa tayari kujaribu vitu vingine na kuanza biashara mpya.
Majaribio elfu 10 ni mbadala sahihi wa masaa elfu 10 kwenye zama tunazoishi sasa ambapo muda ni changamoto kubwa.

Kuruka foleni siyo njia ya mkato.

Kuna ushauri mwingi sana kwenye njia za mkato za kufika kwenye mafanikio.
Lakini ushauri huo huwa siyo sahihi, kwani njia za mkato huwa hazileti matokeo ya kudumu, kwa sababu huwa zinadanganya.
Dhana ya kuruka foleni kupitia majaribio elfu 10 siyo njia ya mkato ya kufanikiwa.
Bali ni kujua yake muhimu ya kuzingatia ili uweze kufika kwenye malengo yako kwa muda mfupi kuliko kusubiri muda mrefu kwenye foleni.

Hakuna mbinu za uongo na za mkato za kufika kwenye mafanikio, lazima uzalishe thamani, lakini pia hulazimiki kusubiri muda mrefu kwenye foleni ili kuja kufanya hivyo.
Unaweza kwenda moja kwa moja kileleni na kutoa thamani kubwa itakayokuwezesha upate unachotaka.

Karibu usome uchambuzi kamili na ushiriki mjadala wa kitabu hiki.

Uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha SKIP THE LINE unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA. karibu ujiunge na channel hiyo ili uweze kusoma uchambuzi huu na uondoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi.

Tutakuwa na mjadala wa moja kwa moja (live) wa kitabu hiki cha SKIP THE LINE kwenye klabu yetu ya kusoma vitabu ya SOMA VITABU TANZANIA.
Mjadala huo utafanyika siku ya jumamosi tarehe 17/07/2021kuanzia saa mbili usiku mpaka saa 4 usiku saa za Afrika Mashariki.
Unaweza kushiriki mjadala huu ukiwa popote duniani, unachohitaji ni mtandao wa intaneti na app ya Telegram Messenger.

Kujiunga na channel na kuweza kushiriki mijadala ya vitabu, tuma ujumbe sasa kwa Telegram kwenda namba 0717 396 253, ujumbe uwe na majina yako, namba yako ya simu na maneno SOMA VITABU.

Karibu usome uchambuzi wa kitabu cha SKIP THE LINE pamoja na vitabu vingine vingi na pia uweze kushiriki mijadala ya klabu ya soma vitabu.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz

Mitandao ya kijamii imekugeuza kuwa mtumwa na kuharibu akili yako. Soma kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI ili uweze kuondoka kwenye utumwa ulionasa. Kukipata wasiliana na 0752 977 170