2389; Usimwamini Yeyote Bila Ya Kitu Hiki…
Edward Deming amewahi kunukuliwa akisema; “In God we trust, all others must bring data.”
Akimaanisha Mungu pekee ndiye wa kumwamini, wengine wote lazima walete data.
Ni kauli rahisi hii, lakini kama ukiielewa na kuiishi, lazima utapiga hatua kubwa kwenye maisha na kile unachofanya.
Usiwe tu mtu wa kuamini kile unachojiambia au unachoambiwa na wengine, badala yake taka kuziona namba.
Kwa kifupi, usiamini bila namba.
Mtu anapokuambia biashara inafanya vizuri, usikimbilie kumuamini kwa sababu ni mtu mwaminifu.
Taka kuziona namba.
Namba huwa hazidanganyi.
Sisi binadamu huwa tunajidanganya kirahisi sana na hadithi zetu mbalimbali.
Na huwa tunaamini kabisa hadithi hizo kama vile ni kweli.
Njia pekee ya kuondokana na udhaifu huo ni kutumia namba. Usiamini kitu bila ya namba.
Unapojiambia huna muda wa kusoma kitabu, au kuandika, au kuanzisha biashara ya pembeni, ni rahisi kuamini hilo.
Lakini jaribu kukaa chini na upime matumizi yako ya muda kwa siku 7 tu, kwa kuandika kila unachofanya kwa kila muda.
Utashangaa jinsi unavyopoteza muda mwingi kwenye maisha yako.
Unaposema kipato chako hakitoshelezi wewe kuweza kuweka akiba, ni rahisi kuamini hilo.
Lakini anza kuhesabu na kuandika kila sentensi inayopita kwenye mikono yako, utashangaa kuona licha ya udogo wa kipato, bado pia umekuwa unakipoteza.
Unasema umejaribu kufanya kila kitu lakini hufanikiwi! Kweli? Hebu orodhesha yote uliyofanya ili uone umefanya mambo elfu ngapi. Huenda hata mia moja hayajafika.
Rafiki, ujumbe ni mfupi na unaoeleweka, wakuaminiwa ni Mungu pekee, wengine wote lazima waonyeshe namba zao.
Zijue namba zako na zitumie kufanya maamuzi yote muhimu kwenye maisha, kazi na biashara zako.
Kama hakuna namba jua kabisa unabahatisha maana kuna mengi hujui.
Kocha.