2421; Siyo kila ushauri unakufaa…
Nianze kwa kusema kila kitu kwenye biashara kinawezekana.
Na kwa biashara yoyote unayofanya, watu watakuja kwako na ushauri wa kila aina.
Na kila ushauri unaopewa utaonekana ni sahihi kabisa na wenye tija kwa biashara.
Lakini siyo kila ushauri unakufaa wewe na biashara yako.
Unapoingia kwenye biashara, unapaswa kuwa na picha kubwa ya wapi unataka biashara hiyo ifike.
Picha hiyo lazima ianzie ndani yako mwenyewe na siyo ya kuiga au kuambiwa na wengine.
Na ukishakuwa na picha hiyo, ndiyo inayopaswa kuganda kwenye fikra zako muda wote.
Unapopewa ushauri na yeyote, angalia kama unakufikisha kwenye picha yako.
Fanyia kazi ule ushauri unaokufikisha kwenye picha kubwa uliyonayo.
Ule ulio kinyume na picha yako achana nao, maana huo utakuwa kikwazo kwako.
Ushauri ni mwingi, tena wa bure kabisa, lakini gharama yake ni pale unapoanza kuutumia.
Wengi wamevuruga biashara zao na kujizuia kukua zaidi kwa kuhangaika na kila ushauri wanaopokea.
Wewe epuka hilo kwa kuchuja kila ushauri kwa kutumia picha kubwa uliyonayo.
Kocha.