2424; Kipi kina nguvu ya kukuzuia?

Kama kuna kitu kina uwezo wa kukuzuia kupata kile unachotaka, basi ukweli ni kwamba hutaweza kukipata.

Kwa sababu dunia huwa siyo nyepesi kutoa kile ambacho mtu anataka, huwa inapima kwanza ni kwa kiasi gani mtu huyo amejitos kukipata.

Kama hujajiambia utapata unachotaka na hakuna chochote kinachoweza kukuzuia, dunia haitakuacha.

Mwanzo kabisa utakutana na magumu, yatakayokutisha na kukupa hofu itakayokuzuia usiendelee.
Hapo tu wengi hukata tamaa na kuacha.

Kuna wabishi ambao watavuka huo ugumu na hao watapokelewa na kikwazo kingine, hiki cha safari hii kinashawishi zaidi.
Maana ni fursa nyingine zinazoonekana nzuri kuliko ile ambayo mtu upo.

Utashawishika kwa kuona kabisa wengine wananufaika, tena kirahisi kuliko wewe.
Utaona kama unajichelewesha kwenye njia uliyochagua wakati njia ya wenzako ni rahisi zaidi.

Ukiteleza tu na kuiacha njia yako, jua tayari umekubali kushindwa. Unapoenda unagundua siyo parahisi kama ulivyoona kwa nje.
Lakini bado haitakuwa rahisi kutoka na kurudi kwenye kile cha awali.

Kwa kifupi unakuwa umevurugwa na kujikuta unakimbizana na mengi mapya kila wakati.

Wapo wanaovuka tamaa ya vingine vizuri, lakini wanakutana na anguko jingine ambalo ni mafanikio madogo.
Watu hao huridhika haraka na mafanikio madogo wanayopata na kujiona kama tayari wameshamaliza kila kitu.

Ile njaa na ya mafanikio waliyokuwa nayo awali inakuwa haipo tena. Wanakosa utayari wa kujifunza waliokuwa nao awali.
Wanakosa hamasa na msukumo kama waliokuwa nao awali.
Hivyo wanakuwa wameyaonja mafanikio, ila kinachofuata ni anguko kubwa.

Kipi kina nguvu ya kukuzuia kupata unachotaka? Maana hicho ndiyo kikwazo kikuu cha mafanikio yako.
Kufanikiwa kweli, lazima ukiri na kutangaza wazi kabisa kwamba hakuna chenye nguvu ya kukuzuia kupata unachotaka.

Kocha.