2469; Kutokumuumiza Yeyote.
Kuna vitu ambavyo huwa tunahangaika navyo kwenye maisha, ambavyo tunajisumbua tu lakini haviwezi kuwa vile tunavyotaka.
Moja ya vitu hivyo ni kutaka kufanya maamuzi ambayo hayatamuumiza mtu yeyote yule.
Hizo ni ndoto ambazo ukiendelea kuziota hutakuja kufanya maamuzi makubwa kwenye maisha yako.
Kwa sababu maamuzi yoyote yale unayofanya kwenye maisha yako, hata yawe mazuri kiasi gani, yataanza kukuumiza wewe mwenyewe.
Halafu yatawaumiza na baadhi ya watu wengine pia.
Sasa kama mtazamo wako ni kutokumuumiza yeyote, hutafanya maamuzi kabisa na hilo litakuwa kikwazo kikubwa kwako kupiga hatua.
Mtu mwingine kuumia na maamuzi yako haimaanishi kwamba siyo sahihi, bali inamaanisha kuna namna alikuwa na mategemeo tofauti.
Sasa kutaka kufanya maamuzi ambayo yataridhisha mategemeo ya kila mmoja ni kujizuia kupiga hatua, kwa sababu mategemeo ya wote huwa hayafanani.
Hupaswi kutumia kigezo cha kutomuumiza mtu kwenye kufanya maamuzi.
Badala yake tumia misingi mikuu miwili.
Msingi wa kwanza ni kufanya kilicho sahihi. Mara zote fanya kile kilicho sahihi maana hicho ndiyo chenye manufaa. Kitakuwa na maumivu kwa baadhi ya watu, lakini kitakuwa na manufaa makubwa baadaye.
Msingi wa pili ni kupunguza majuto. Mara zote fanya kile ambacho hutakuja kujutia sana baadaye. Hakuna kinachoumiza kama majuto, pale unapojikuta ukisema kama ninge…
Jiulize kipi ambacho utajutia sana baadaye kama utafanya au hutafanya kitu, kisha fanya maamuzi ambayo yatapunguza majuto hayo.
Hatua ya kuchukua;
Kama kuna maamuzi ambayo umekuwa unaahirisha kuyafanya kwa sababu hutaki yeyote aumie, jua unajichelewesha au unatumia kama kisingizio. Leo yapitie maamuzi hayo, jua ni kitu kipi kilicho sahihi kufanya na ambacho kitakupunguzia wewe majuto. Kisha fanya maamuzi yako ukijua hakuna namna utaweza kuepuka baadhi ya watu kuumia.
Tafakari;
Hakuna kitu chochote unachoweza kufanya kwenye maisha na ukakubalika na watu wote. Hakuna maamuzi yoyote unayoweza kufanya na yasiwaumize baadhi ya watu. Fanya kilicho sahihi na punguza majuto kwa upande wako.
Kocha.