2497; Muda, Nguvu, Umakini.

Rasilimali kubwa tatu unazopaswa kuzitunza na kuzitumia vizuri kama unayataka mafanikio makubwa.

Tumezoea kuona msisitizo ukiwekwa sana kwenye muda, jinsi ya kudhibiti na kutumia muda vizuri ili kuweza kufanya makubwa.

Lakini siyo muda pekee ambao ndiyo rasilimali yenye uhaba na muhimu kwa mafanikio yako.

Kuna nguvu za mwili wako, ambazo nazo zina ukomo. Unapoianza siku unakuwa na nguvu kubwa, lakini kila unapofanya kitu unapunguza nguvu hizo.
Ukihangaika na mambo yasiyo muhimu yananyonya nguvu zako na kukuacha ukiwa umechoka, ukiwa huwezi kufanya mengine makubwa.

Kuna umakini wa akili yako, huu nao ni muhimu kwa sababu huwa unachoka haraka. Kadiri unavyoutawanya umakini wako kwenye mambo mengi ndivyo unavyoendelea kupungua na kushindwa kufanya makubwa.
Hivyo unapaswa kuweka umakini wako wote kwenye mambo machache muhimu ili kuzalisha matokeo bora.

Na muda huo unajulikana, kuna masaa 24 pekee kwenye siku yako, huwezi kuongeza hata sekunde moja. Hivyo unapochagua kufanya kitu fulani, maana yake huo muda huwezi kuutumia kufanya kitu kingine.

Kitu kikubwa na muhimu sana kwenye rasilimali hizi tatu ni hiki; kwenye kila siku yako utatumia rasilimali hizo, iwe unafanya makubwa au madogo, mazuri au mabaya.
Masaa 24 ya kila siku yatapita, nguvu zako za siku zitaisha na kubaki ukiwa umechoka na umakini wako utatumika.

Hivyo badala ya kupoteza rasilimali hizo muhimu kila siku kwenye mambo yasiyo na tija, ni vyema ukachagua kuziwekeza kwenye maeneo ambayo yanaweza kuzalisha matokeo makubwa na kukuwezesha kufanikiwa.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapoianza siku yako, pangilia kabisha jinsi unavyokwenda kutumia rasilimali hizo tatu muhimu, kwa namna ambayo itakufikisha kwenye mafanikio unayoyataka.
Usikubali rasilimali hizi zitumike tu hovyo. Panga unatumiaje muda wako, nguvu zako na umakini wako.
Na unapofanya kitu chochote, jiulize kwanza je haya ndiyo matumizi bora kabisa ya rasilimali zangu muhimu? Kama jibu ni ndiyo endelea, kama siyo acha.

Tafakari;
Kama rasilimali zitatumiwa tu, basi ni vyema ukazitumia kwa namna yenye manufaa zaidi kwako.
Kama gari yenye uwezo wa kubeba tani 10 za mzigo lazima itoke Dar kwenda Dodoma, ni vyema kubeba tani 10 za mzigo kuliko kubeba tani ya mzigo. Maana rasilimali zinazotumika ni zile zile, iwe utabeba tani moja au kumi.

Kocha.