Utangulizi wa sheria za siku.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye mwaka wa mafanikio 2021/2022 kila siku tutaipata sheria ya siku kutoka kwenye kitabu kinachoitwa The daily laws : 366 meditations on power, seduction, mastery, strategy, and human nature kilichoandikwa na Robert Greene.

Robert Greene ambaye ni mwandishi aliyebobea kwenye sheria za madaraka na sheria za asili za binadamu, ameandika kitabu hiki kutokana na uzoefu wake wa zaidi ya miaka 20 ya kutafiti na kufanyia kazi kwenye eneo hilo.

Kutoka kwenye vitabu vyake mashuhuri kama 48 Laws Of Power, Mastery, Art Of Seduction, 33 Strategies of War na Laws of human nature, Robert anatupa mwongozo wa kuendesha maisha yetu ya kila siku kwa namna ambayo tutaepuka kutumiwa vibaya na watu wenye nia mbaya ya kujinufaisha kupitia sisi.

Pia sheria hizi zinatusaidia kujitambua sisi wenyewe na kuweza kufikia ubobezi wa juu kwenye wito wetu kitu kitakachotuwezesha kufanya makubwa na kuacha alama kubwa pia.

Kitabu kimepangiliwa kwa namna ya kuwa na sheria ya kila siku kwa siku zote 366 za mwaka.
Hivyo kila siku tutaipata sheria ya siku kutoka kwenye kitabu.

Japo mwaka wetu wa mafanikio unaanza Novemba, tutaanzia kwenye mwezi januari wa kitabu kwa sababu miezi ya mwanzo ni ya kujitambua, kulijua kusudi na kujenga ubobezi.

Miezi mitatu ya mwanzo itatusaidia kuondokana na kelele za nje zinazotuambia nini tunapaswa kufanya na kutuwezesha kusikiliza sauti ya ndani yetu ambayo ndiyo sauti sahihi inayojua nini hasa tunachotaka.

Miezi mitatu inayofuata itakuwezesha kuziona siasa zinazoendelea kwenye maeneo ya kazi na biashara na jinsi ya kuzizuia zisiwe kikwazo kwako. Utaona jinsi baadhi ya watu walivyo na ushawishi mbaya ili kukutumia wewe kupata wanachotaka.

Miezi mitatu inayofuata itakufundisha jinsi ushawishi unavyofanya kazi. Hii itakusaidia kuweza kuwashawishi wengine kukubaliana na wewe kwenye mambo mbalimbali.

Miezi mitatu ya mwisho itakufundisha motisha mkuu unaowasukuma binadamu kwenye yale wanayofanya. Hii itakusaidia kuwaelewa binadamu na hata wewe mwenyewe na kuweza kuwachukulia watu jinsi walivyo.

Kwa ujumla, sheria hizi za siku zinatusaidia kujitambua sisi wenyewe, kuwaelewa wengine na kuweza kuchangamana na kushirikiana nao kwa namna ambayo ni bora kwetu.

Karibu sana kwenye kujifunza sheria hizi za siku kila siku na uchukue hatua ili ushike hatamu ya maisha yako na kuweza kufanya makubwa zaidi.

Kocha.