#SheriaYaLeo (4/366); Tayari Iko Ndani Yako.

Kujua wito na kusudi la maisha yako, huhitaji kwenda kutafuta mahali popote pale.
Tayari hilo lipo ndani yako.

Kama bado hujajua ni kwa sababu imefukiwa na miaka mingi uliyoishi kwa kupuuza kile kilicho ndani yako.
Hivyo unachopaswa kufanya sasa ni kuchimba kile kilicho ndani yako, ili kuweza kukifikia na kukiishi.

Kumbuka vitu ambavyo ulikuwa unapata msukumo mkubwa wa kuvifanya.
Vitu ambavyo ulikuwa tayari kurudia kuvifanya kwa muda mrefu bila kuchoka.
Vitu ambavyo viliibua udadisi mkubwa ndani yako.

Huhitaji kubuni au kutengeneza vitu hivyo, tayari vipo ndani yako.
Huhitaji Kutengeneza chochote kipya, unachohitaji ni kuchimba ndani yako na kufikia kile halisi kwako, ambacho kitaibua maisha mapya kwako.

Sheria ya leo; Waulize watu wanaokumbuka utoto wako wakuambie nini ulikuwa unapendelea sana. Rudi kufanya vitu hivyo ulivyopendelea sana utotoni.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma