Rafiki yangu mpendwa,
Ukiwa hujafanikiwa, watu wengi watakupenda na kukuonea huruma.
Hiyo ni kwa sababu unakuwa huna hatari yoyote kubwa kwao.
Na pia wanajua wanaweza kukutumia wakati wowote wanapotaka kwa manufaa yao.

Unapoanzia chini ni rahisi kuamini mambo yatakwenda hivyo wakati wote, watu wataendelea kukujali na kukuonea huruma kadiri unavyofanikiwa. Hasa ukizingatia magumu unayoyapitia katika kuyatafuta mafanikio yako.

Lakini hilo siyo linalotokea, mambo hayaendi hivyo. Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyojua tabia halisi za watu.
Kwa asili, watu huwa hawawapendi wale waliofanikiwa kuzidi wao.
Wanawaona ni hatari kubwa kwao na hawawezi kuwatumia kwa namna wanavyotaka wao wenyewe.

Hasa pale mtu anayefanikiwa anapokuwa alianzia chini ya wengine, wale waliokuwa juu yake kabla hujafanikiwa hawatakubali kumwachia kirahisi aendelee kufanikiwa, maana wanajua ataondoka chini yao na kuwa juu yao.

Hivyo unapopambana kufanikiwa, kuna ambao watakuwa wanapambana kukuangusha, kukuzuia usifanikiwe kuwazidi.
Watu hao wanaitwa wasawazishaji au kwa kiingereza levellers.
Lengo lao kubwa ni kuhakikisha hakuna anayewazidi wengine, kwamba watu wote wanakuwa kwenye ngazi sawa.

Watu hawa huona wana sababu za msingi kabisa kufanya hivyo, kwa kuamini wanaondoa matabaka.
Lakini ambacho wanaficha ni nia yao ya ndani ya kutaka watu wabaki chini ya udhibiti wao.
Wanajua kadiri watu wanavyofanikiwa ndivyo wanavyokuwa huru na kutolazimika kufuata yale wasiyokubaliana nayo.

Jamii zetu zimejaa watu wa aina hii, wengine wapo kwenye hili kundi bila hata ya kujua kwamba wapo kwenye kundi hilo.

Wajibu wako mkubwa kwenye maisha kama ambavyo unayapambania mafanikio yako ni kuwajua wasawazishaji na kuwazuia wasiwe kikwazo kwenye mafanikio yako.

Kwa kuanza mchukulie kila mtu ni msawazishaji, mpaka pale utakapojiridhisha siyo msawazishaji.
Ukweli ni kwamba kadiri unavyofanikiwa, wengi wanaokujua na wanaokuzunguka hawatafurahishwa na mafanikio yako.
Wengine wataona wanastahili kuwa sehemu ya mafanikio yako japo hawajaweka mchango mkubwa.
Wote hao waweke kwenye kundi la wasawazishaji.

Kitu cha pili usiweke mambo yako wazi sana kadiri unavyofanikiwa.
Jamii huwa inatuhadaa tujisifu kwa mafanikio yetu na hapo kuingia kwenye mtego wa kuweka kila kitu chetu wazi.
Kadiri watu wanavyojua mambo mengi kuhusu wewe ndivyo wanavyopata fursa nyingi za kukuvuruga na kuwa kikwazo kwako.

Hakikisha sehemu kubwa ya mafanikio yako ambayo inaweza kutokuonekana basi haionekani.
Wape watu sababu za kukudharau na kuuchukulia poa, itawafanya wakuone siyo hatari na hivyo kutohangaika kukuangusha.

Watu wengi wamekuwa wanakaribisha matatizo kwao wenyewe kwa kuweka wazi mambo yao mengi kiasi cha kuibua wivu na chuki kwa wengine.
Wewe usiwe hivyo, hakikisha chochote ambacho watu wanaweza kutokukijua basi hawakijui.

Mwisho kuwa mnyenyekevu mara zote. Kiburi na majigambo vimewaponza wengi. Kutaka kujionyesha imekuwa sumu kubwa kwa wengi.
Wewe kuwa mnyenyekevu, watu wasione tofauti yako kitabia kabla na baada ya kufanikiwa.
Endelea kuwa mtu wa kujifunza na endelea kuwa mtu wa kuweka juhudi kubwa kwenye kila unachofanya.
Kadiri unavyotoa thamani zaidi na kadiri unavyojali kile unachofanya, ndivyo wengi watakukubali na kutokujali sana kuhusu mafanikio yako.

Ukiyapata mafanikio na kisha kuacha kuweka juhudi huku ukiwa na kiburi na majigambo, watu watapata kila sababu ya kukushambulia na kukuangusha.

Pamoja na yote haya, usisahau kuishi maisha halisi kwako, usiishi maisha ya kuigiza ili tu kuwafurahisha wengine.
Jua huwezi kumfurahisha na kumridhisha kila mtu.
Hivyo weka juhudi zako kwenye kuishi maisha halisi kwako, wanaokuelewa wataenda na wewe na wasiokuelewa hawatajali.

Hakikisha unapata na kusoma kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO, kitabu ambacho kinakupa majibu yote ya kutafuta na kuyatunza mafanikio.
Unayakosa mafanikio kwa sababu kuna kanuni za msingi kabisa ambazo umekuwa unazipuuza.
Usiendelee tena kuwa kikwazo kwako mwenyewe, pata nakala ya kitabu hiki leo na uishi kwa kanuni sahihi ili ufanikiwe.
Kupata kitabu hiki wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa ulipo.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz