Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi ambao wanaingia kwenye biashara, wamekuwa wanafanya hivyo kwa msukumo wa kutengeneza kipato cha ziada. Lakini wengi wamekuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu biashara wanazoendesha.

Wengi wanaamini wakishakuwa na mtaji, na wakiwa na kitu wanachouza, basi wateja watakuja wenyewe. Hii ni njia rahisi ya kuifikiria biashara, lakini biashara nyingi sana zinakufa huku wamiliki wakiwa na mtaji na bidhaa au huduma wanazotoa.

Ili biashara ambayo unafanya iweze kufanikiwa, inapaswa kuwa na sifa ambazo zinachochea mafanikio ya biashara hiyo. Sifa hizo zinaiweka biashara kwenye nafasi nzuri ya kuweza kufanikiwa.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha sifa tano unazohitaji kujenga kwenye biashara yako ili iweze kufanikiwa.

  1. Urahisi wa biashara kueleweka.

Kama biashara ni rahisi kueleweka na yeyote, biashara hiyo ina nafasi kubwa sana ya kufanikiwa. Kwa sababu ni rahisi kwa mfanyabiashara kumshawishi mteja anunue kama ni rahisi kwa mteja kuelewa nini ananunua na kinamsaidia nini.

Nimekuwa nasema kama biashara unayofanya au unayotaka kufanya huwezi kumweleza mtoto wa darasa la tano na akaelewa, basi huijui vizuri biashara hiyo na itakuwa kikwazo kwako kufanikiwa.

Ingia kwenye biashara ambayo ni rahisi kwako kuelewa na hata kuwaelezea wengine na utaweza kuuza zaidi na kufanikiwa.

  1. Wateja wanaojirudia.

Mteja akinunua mara moja kwenye biashara yako na asirudi tena, ni hasara kwa biashara yako. Hivyo kama una biashara ambayo ina wateja wanaojirudia, upo kwenye nafasi nzuri zaidi ya mafanikio.

Unahitaji kuwa kwenye biashara ambayo chochote unachouza, mteja anahitaji kununua tena na tena na tena. Na akishanunua, mpe sababu ya kurudi kununua tena kwako.

Mteja ambaye tayari alishanunua kwako, kama utamuuzia vizuri, ni rahisi zaidi kwake kununua tena kuliko mteja ambaye hajawahi kununua tena. Hivyo unapomuuzia mteja, hakikisha unampa sababu ya kurudi tena.

SOMA; Biashara Kumi (10) Unazoweza Kuanzisha Mwaka Huu 2018 Na Ukapata Mafanikio Makubwa.

  1. Bidhaa/huduma zisizoharibika haraka.

Sifa nyingine muhimu ya biashara zinazofanikiwa ni muda ambao bidhaa au huduma inaweza kukaa bila ya kuharibika. Kadiri unavyoweza kutunza huduma na bidhaa unazotoa kwa muda mrefu, ndivyo inavyowapa wateja nafasi ya kununua zaidi na biashara kufanikiwa.

Kama bidhaa au huduma unazotoa zinaharibika au kumaliza ubora wake haraka, utajikuta unasukumwa kuuza hata kwa hasara ili usibaki na vitu vinavyoharibika.

  1. Urahisi wa kumfikia mteja.

Biashara zenye mafanikio ni zile ambazo zinaweza kumfikia mteja kwa urahisi zaidi. Na inaweza kuwa kwa biashara kuwa karibu zaidi na wateja wake, au kuwa na mfumo wa kuwafikishia wateja kile wanachohitaji.

Kwa kipindi cha nyuma, biashara iliyokuwa eneo linalopita watu wengi ilikuwa na mafanikio makubwa kuliko iliyokuwa eneo lisilokuwa na watu wengi.

Lakini kwenye zama hizi za mtandao, biashara inaweza kuwa popote na kwa kutumia nguvu ya mtandao ukaweza kuwafikia wateja kule walipo. Wakaagiza kwa njia ya mtandao na wakapelekewa walichoagiza.

Rahisisha ufikiaji wa wateja wa biashara yako na utaweza kuikuza zaidi biashara yako.

  1. Uwezekano wa biashara kukua zaidi.

Ili biashara iweze kufanikiwa, ni lazima iweze kukua zaidi ya pale ilipo sasa. Kwa ukuaji inamaanisha kuwa na wateja wengi kuliko ilivyoanza, kuwa na bidhaa au huduma zaidi ya ilivyoanza na hata kuwa na matawi mengi zaidi.

Kama biashara ina bidhaa au huduma moja pekee, na inategemea aina fulani ya wateja tu, na huku inataka uwepo wa mwanzilishi wa biashara tu inakuwa na ukomo wa kukua.

Iweke biashara yako kwenye nafasi ya kukua zaidi kwa kutafuta wateja wapya kila mara, kuongeza bidhaa au huduma zinazoendana na unachouza sasa na pia kwa kutengeneza mfumo ambao biashara inaweza kujiendesha hata kama haupo moja kwa moja kwenye biashara hiyo.

Rafiki, usiendeshe tena biashara yako kwa mazoea, badala yake endesha ukiwa na ndoto na maono makubwa ya kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara hiyo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha