Rafiki yangu mpendwa,

Juma la mafanikio namba 34 kwa mwaka huu 2018 linatuacha sasa. Ni juma ambalo nina imani limekuwa bora sana kwako, kuanzia kwenye kujifunza na kuchukua hatua kubwa. Na hata kama hujapata matokeo makubwa, basi umejifunza na umejenga msingi mzuri kwa ajili ya mafanikio yako.

Kama unaijua hadithi ya mbuyu, wanasema mbegu ya mbuyu inachukua miaka kuchomoza, lakini ikishaanza kuchomoza, ukuaji wake unakuwa wa kasi sana. Kipindi chote ambacho ukuaji haukuwa unaonekana, siyo kwamba mbegu hiyo ilikuwa haikui, bali ilikuwa inakua na kutengeneza ukuaji wa baadaye wa haraka.

Kadhalika kwenye maisha yako na kazi zako, pale unapoweka juhudi kubwa lakini hupati matokeo makubwa unayotarajia, usikate tamaa na kuona unapoteza nguvu unazoweka. Badala yake endelea kuweka juhudi kwa sababu zinaendelea kutengeneza matokeo makubwa ya baadaye.

Kuna siku matokeo makubwa yataonekana kwa haraka, na wasiojua watasema una bahati sana. Wasichojua ni kwamba kuna kipindi ulisota sana bila ya kuona mafanikio ambayo wakati huo yanaonekana kwa urahisi sana.

Endelea kuweka juhudi rafiki, na mara zote fuata kanuni yetu ya MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Karibu kwenye TANO ZA JUMA ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kujifunza, kutafakari na kuhamasika kuchukua hatua zaidi ili kuweza kufanikiwa zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; FUNGUO ZA USTADI NA MAFANIKIO.

Ukiwaangalia watu wote ambao wamefikia mafanikio makubwa na ya kweli, mafanikio yanayodumu, wamefikia ustadi wa hali ya juu kwenye kile wanachofanya. Yaani wanakuwa wamebobea kiasi kwamba kwao kile wanachofanya siyo kazi tena bali ni sehemu ya maisha yao.

Sasa kuna vitabu vingi sana vimeandika jinsi ya kufikia ubobezi wa hali ya juu kwenye jambo lolote. Lakini vitabu vingi vinavyoelezea ubobezi vimesheheni hasa, yaani ni vitabu vikubwa, ambavyo vimejadili ustadi na ubobezi kwa kina kiasi kwamba ukisoma, unaona namna ambavyo ubobezi siyo kitu rahisi.

Lakini juma hili nilikutana na kitabu cha George Leonard kinachoitwa MASTERY: KEYS TO SUCCESS AND LONG-TERM FULFILLMENT. Kitabu hiki naweza kusema ni moja ya vitabu ambavyo vimeelezea ubobezi kwa lugha rahisi na kwa namna ambayo kila mtu anaweza kuelewa na kuchukua hatua.

George ambaye ni mbobezi kwenye mchezo wa AIKIDO, anatushirikisha namna ambavyo kila mmoja wetu anaweza kufikia ubobezi na mafanikio makubwa kwenye eneo lolote la maisha. Kuanzia kwenye kazi, biashara, michezo, mahusiano, masomo, sanaa na kadhalika.

Kwenye kitabu hiki, George ametushirikisha mambo matatu muhimu kwenye safari ya ubobezi.

MOJA; SAFARI YA UBOBEZI.

George anatuambia kwamba safari ya ubobezi siyo rahisi, lakini pia siyo kwamba haiwezekani.

Vitu vinavyofanya safari hii ngumu ni wengi kukosa utayari unaohitajika ili kufikia ubobezi, ambao ni muda mrefu na kuweka kazi hasa. Kitu cha pili ni jamii inayomzunguka mtu. Angalia tv, ingia mtandaoni na hata fuatilia habari yoyote, utaona jinsi ambavyo mafanikio ya haraka yanavyotukuzwa na kushangiliwa. Hapo hujasikia kuhusu bahati nasibu na kamari ambazo watu wanahamasishwa wacheze ili wafanikiwe haraka. Kila mtu anakazana kutafuta njia ya mkato ya kufanikiwa, ambayo inaweza kumpa mtu kile anachotaka, lakini haiwezi kumpa ubobezi wala mafanikio ya kudumu.

Hivyo kama unataka kubebea kwenye kitu chochote, vitu hivi viwili havikwepeki; MUDA NA KAZI.

Zipo njia tatu ambazo mwandishi anatuambia wengi hupotea kwenye njia hizo badala ya kufuata njia ya ubobezi, ambayo inaonekana ngumu na inayohitaji kazi na muda.

Njia ya kwanza ni ya kutangatanga. Hapa mtu anaanza kitu, akiwa na hamasa kubwa na anaweka juhudi kubwa, baada ya muda hamasa zinaisha kabisa na anaacha. Anaanza tena kitu kingine akiwa na hamasa kubwa, mwanzoni anaweka juhudi sana lakini haichukui muda, hamasa inaisha na anaenda kwenye kitu kingine. Watu wa aina hii utawakuta wameanzisha vitu vingi lakini hakuna hata kimoja wamefikia mafanikio makubwa. Na vingi wanaishia njiani.

Njia ya pili ni kuishia njiani. Hapa mtu anaanzisha kitu, anaweka juhudi kubwa sana mwanzoni, anapata matokeo makubwa sana, lakini pale anapofikia kwenye kilele ambacho wengi wanaona mafanikio ndiyo makubwa zaidi kwake, anaishia hapo na kinachofuatia ni kuporomoka. Hapa mtu anaweka juhudi kubwa sana mwanzoni, ambazo zinaleta matokeo makubwa, lakini haziwezi kuwa endelevu. Hivyo mtu anaonja mafanikio lakini anapotea kabisa baada ya mafanikio hayo.

Njia ya tatu ni mazoea. Hapa mtu anachagua kufanya kitu, anaweka juhudi kiasi mwanzoni, anapiga hatua na baada ya hapo anafanya kwa mazoea kwa maisha yake yote. Hapati mafanikio makubwa na wala hashuki chini, anakuwa anaenda kwa mazoea, ambayo hayampi mafanikio makubwa zaidi.

Je wewe ni njia ipi inakupoteza kwenye ubobezi?

MBILI; FUNGUO KUU TANO ZA KUFIKIA UBOBEZI.

Ufunguo wa kwanza; maelekezo.

Huwezi kufikia ubobezi kama haupo tayari kupokea maelekezo. Lazima uwe tayari kujifunza na lazima uwe tayari kufundishika. Lazima uwe na mwalimu au njia ya kujifunza ambayo unaiamini na kuifuata.

Kama hutamwamini mwalimu au njia ya kujifunza uliyochagua, itakuwa vigumu sana kwako kufikia ubobezi.

Ufunguo wa pili; mazoezi.

Ukishajifunza, lazima uchukue hatua, la sivyo kujifunza hakutakuwa na maana yoyote kwako. Lazima uwe tayari kuchukua hatua kubwa sana ili uweze kupiga hatua zaidi.

Kadiri unavyotaka kufika juu zaidi, ndivyo unavyohitaji kuchukua hatua zaidi.

Ufunguo wa tatu; kujisalimisha.

Changamoto ya wengi kwenye kufikia ubobezi na hata mafanikio ni kwamba, wakipiga hatua kidogo basi wanaanza kuwa na dharau, na kuona tayari wanajua, hakuna tena wa kuwafundisha au kuwaambia ni nini cha kufanya.

Mbobezi ni yule ambaye yupo tayari kuendelea kujifunza kama vile ndiyo anaanza. Ili ubobee lazima uweze kujishusha na kujisalimisha kwa walimu wako na haya kwenye kuchukua hatua. Ukishaanza kujiona unajua zaidi ya wengine, au hakuna kipya unaweza kujifunza, lazima upotee.

Ufunguo wa nne; kuwa na nia.

Tofauti ya aliyebobea na anayeanza ni hii; aliyebobea anafanya kitu kwa muda aliopanga kufanya, iwe anajisikia au hajisikii. Anayeanza, anafanya kitu pale anapojisikia kufanya.

Katika kubobea, lazima uwe tayari kuongozwa na nia yako mwenyewe na siyo hisia zako. Unachagua kufanya kitu na unafanya kama ulivyopanga na siyo kujiambia kama unajisikia kufanya au la.

Ufunguo wa tano; kujiweka kwenye hatari mara zote.

Mafanikio madogo huwa ni kikwazo cha mafanikio makubwa. Watu wanapofanikiwa kidogo, badala ya kukazana wafanikiwe zaidi, wanakazana kulinda mafanikio waliyopata. Ni sawa na timu ya mpira inayoingia uwanjani, inashambulia, inapata goli moja la kuongoza. Baada ya hapo timu inaacha kushambulia na wanachofanya ni kulinda wasifungwe. Kila mtu anajua, timu za aina hii huishia kushindwa.

Unapopiga hatua kwenye safari yako ya ubobezi na mafanikio, unahitaji kujiweka kwenye hali ya hatari mara zote. Japokuwa unakuwa umefika juu, jiweke kwenye hali ya hatari kama vile ndiyo unaanza. Jaribu vitu ambavyo ni vipya kwako hata kama vile ulivyozoea vinafanya vizuri. Unapokuwa kwenye hali ya hatari, akili yako inafikiri vizuri zaidi na unakuwa tayari kuchukua hatua zaidi.

TATU; ZANA ZA SAFARI YA UBOBEZI.

Safari hii ni ngumu, hivyo bila ya zana sahihi, itakuwa ngumu kwako.

George ametushirikisha zana muhimu sana kwenye safari ya ubobezi na mafanikio makubwa.

Kitu cha kwanza muhimu kabisa unahitaji kufanya maamuzi nini unataka na kukata shauri kwamba hicho ndiyo utafanyia kazi. Huwezi kufikia ubobezi na mafanikio makubwa kwa kuhangaika na kila kitu. Lazima uchague kitu kimoja au vichache na kuacha na mengine yote. usiwe mtu w akukimbizana na kila aina ya fursa mpya.

Kitu cha pili unahitaji kuwa na nguvu za kuweza kuimudu safari hii. Bila ya nguvu, na mwili wenye afya bora, pamoja na akili iliyotulia, utachemsha kwenye safari hii nzito. Kitu kimoja ambacho mwandishi anatuambia kwenye nguvu ni kwamba, mwili unatengeneza nguvu kama ukitumia nguvu. Kwa mfano kama hufanyi chochote, umekaa tu, utajisikia kuchoka sana. Lakini kama utaamka na kukimbia, utashangaa kwamba unakuwa na nguvu na uchovu unaondoka kabisa. Hivyo miili yetu inatengeneza nguvu pale tunapotumia nguvu. Afya zetu ni kitu cha kwanza tunapaswa kulinda sana kwenye safari yetu ya ubobezi na mafanikio. Hivyo ulaji, kufanya mazoezi na hata kupumzika ni vitu muhimu kwenye safari hii.

Zana ya mwisho ambayo mwandishi ametupa ni kuepuka vikwazo ambavyo vipo kwenye safari yetu ya ubobezi. Vikwazo hivyo ni migogoro yako binafsi na wengine pia, kukazana na malengo ambayo hayakusaidii kufikia ubobezi, kupata mafunzo yasiyo sahihi, kukosa ushindani, kushindana kupita kiasi, uvivu, maumivu, madawa na vilevi, ushindi na zawadi, ubatili, kukosa msimamo na kutaka ukamilifu.

Rafiki yangu, napenda sana wewe ufanikiwe kwa viwango vya hali ya juu sana, napenda sana wewe ubobe kwenye chochote unachofanya, kwa sababu najua kiwango chako cha mafanikio ndiyo kitakuwa kiwango changu cha mafanikio pia. Hivyo ishi misingi hii ya ubobezi, pata muda na usome kitabu hichi na uendelee kuweka juhudi kwenye kile ulichochagua kufanya, na hakuna kitakachokuzuia usifanikiwe. Na kama bado hujajiunga kwenye KISIMA CHA MAARIFA, mahali sahihi kwa wale wanaosaka mafanikio makubwa, basi unakosa mengi, karibu sana.

Kitabu hichi na vingine ninavyoshirikisha kwenye hizi tano za juma ninaviweka kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Ukiwa mwanachama unapakua na kujisomea, na pia unaweza kuwasiliana na mimi moja kwa moja na tukajadili kwa kina zaidi jinsi ya kuishi misingi hii ya ubobezi.

#2 MAKALA YA WIKI; SAA MOJA MUHIMU SANA KWENYE SIKU YAKO.

Rafiki yangu, kuna kitu kimoja ambacho nimekuwa sikielewi kwenye muda. Watu ambao hawana kitu cha msingi wanafanya na muda wao ndiyo wako bize mno, wanakazana na kila kitu. Lakini wale ambao wana mambo muhimu sana wanafanya na muda wao, ndiyo watu ambao wana muda mwingi mno.

Mtu mmoja amewahi kusema, ukitaka kitu chako kifanyike, mpe mtu ambaye hana kabisa muda wa kufanya, kwa hakika ukimshawishi na akakubali, atafanya. Lakini ukimpa yule ambaye anakuambia ana muda wa kutosha, utaishia kupokea sababu kwa nini bado hajamaliza kufanya.

Juma hili nimekushirikisha makala kuhusu saa moja muhimu sana kwenye siku yako, ambayo ukiweza kuitawala na kuisimamia saa hiyo moja, umeshinda kwenye siku yako hiyo. Lakini kama utaipoteza saa hii moja, hakuna kikubwa utaweza kufanya kwenye siku yako.

Niseme tu kwamba kama hujasoma makala hiyo ya saa moja muhimu kwa maisha yako, acha kila unachofanya na isome sasa. Maana unakazana na mbio ambazo zinazidi kukupoteza. Soma makala hiyo hapa; Hii Ndiyo Saa Takatifu Kwenye Kila Siku Ya Maisha Yako, Unayopaswa Kuilinda Na Kuitumia Vizuri Kama Unataka Mafanikio Makubwa.

Bila ya kusahau, kuna makala nyingine nzuri sana nilikuandalia juma hili kuhusu sifa tano za biashara inayoweza kufikia mafanikio makubwa. Soma hapa kujua kama biashara yako ina sifa hizi tano; Sifa Tano (5) Za Biashara Inayoweza Kufikia Mafanikio Makubwa.

#3 TUONGEE PESA; JE FEDHA INAWEZA KUTATUA?

Mfanyabiashara, mwekezaji na mwandishi Kevin O’Leary anasema kwenye maisha kuna wanaume, wanawake na fedha. Anasema shida yoyote kwenye maisha, inatokana na vitu hivyo vitatu. Na pia anasema, sehemu kubwa ya matatizo ya wengi, inatokana na ukosefu wa fedha, au tabia mbaya kwenye fedha.

Kwenye tuongee pesa leo, nataka ujiulize swali hili muhimu sana. Unapokuwa na tatizo lolote kwenye maisha yako, jiulize je nikiwa na fedha zaidi tatizo hili linatatuliwa. Kama jibu ni ndiyo, basi huhitaji kuendelea kuumia, badala yake kaa chini na ona njia zipi unaweza kutumia kupata fedha unazohitaji ili kutatua tatizo hilo. Na ukishachagua njia unayotumia, weka kazi na usipoteze muda kwenye lolote.

Na pia kama jibu likiwa hapana, kwamba fedha haiwezi kutatua tatizo ulilonalo, hapo kabisa ndiyo huhitaji kuwa na wasiwasi wala kujitesa. Maana kama fedha ziadi haiwezi kutatua, basi unahitaji kuachia muda.

Kumbuka kwenye maisha kuna wanaume, wanawake na fedha. Kama fedha inaweza kutatua tatizo, usijiumize, badala yake tafuta fedha na tatua tatizo hilo.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; UMESHAJIHAKIKISHIA NAFASI YA KUSHIRIKI SEMINA YA 2018?

Kila mwaka, nimekuwa naandaa semina moja ya kukutana ana kwa ana, semina ya KISIMA CHA MAARIFA.

Mwaka huu, semina itafanyika tarehe 03/11/2018.

Swali langu kwako ni je umeshajiwekea nafasi ya kushiriki semina hii. Kama bado basi tuma ujumbe sasa kwa njia ya wasap namba 0717396253 wenye majina yako kamili, namba ya simu na maelezo kwamba utashiriki semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Ada ya kushiriki semina hii ni tsh 100,000/= na mwisho wa kulipa ni tarehe 31/10/2018. Unaweza kuchagua kulipa kidogo kidogo kila siku, kila wiki na kila mwezi. Au unaweza kulipa yote kwa pamoja kabla ya tarehe hiyo ya mwisho kulipia.

Karibu sana tukutane wanamafanikio wote kwa pamoja, tujifunze, kuhamasika na kuweza kuchukua hatua kubwa zaidi ili kufanikiwa zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; USIWE MPUMBAVU KWENYE USINGIZI.

‘When Napoleon Bonaparte was asked how many hours of sleep a person should have each night, he replied “Six for a man, seven for a woman, eight for a fool.’ – Napoleon Bonaparte

Napoleon Bonaparte, aliyekuwa mtawala wa ufaransa na jenerali wa kivita, alipoulizwa ni masaa mangapi mtu anapaswa kulala kwa usiku alijibu, MASAA SITA KWA MWANAUME, SABA KWA MWANAMKE NA NANE KWA MPUMBAVU.

Uh, ni kauli kali sana hiyo, lakini yeye uzito wa kipekee. Na niseme siyo kauli inayowafaa wote, kwa sababu watu wengi, wenye maisha ya kawaida, wanapata masaa 8 ya kazi, 8 ya kupumzika na 8 ya kulala. Sasa kama unataka mafanikio makubwa, usijidanganye kwamba kwa masaa 8 tu ya kazi unaweza kufika mafanikio hayo makubwa.

Unahitaji kupunguza masaa mengi kwenye hayo maeneo mengine, na hivyo kupunguza saa moja au mbili kwenye muda wa kulala itakuwa jambo sahihi kwako.

Nimalizie kwa kusema kwamba, kama unataka mafanikio makubwa, kulala masaa 8 na kuendelea ni kujidanganya. Kwa sababu muda unaopoteza kwenye kulala, ni muda ambao kama ungeweza kuutumia vyema ungepiga hatua sana. Halafu kama unasema huna muda na huku unalala zaidi, unakuwa unamdanganya nani?

Rafiki, juma namna 34 limetuaga, lakini ni vizuri tuna juma namba 35 lipo mbele yetu, juma la mafanikio, juma la kufanya makubwa zaidi. Jifunze, na anza kuchukua hatua ili juma la 35 liwe bora zaidi kwako.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu