Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi sana wanaingia kwenye biashara kwa sababu zisizo sahihi. Wanaingia kwenye biashara wakitafuta vitu ambavyo siyo sahihi kwao, na wanaingia kwenye biashara ambazo siyo sahihi kwao. Wanakazana sana kwenye biashara hizo lakini hawapigi hatua kubwa.
Biashara yoyote ile inaweza kumletea mtu anayeifanya mafanikio makubwa, lakini ni kama mtu anayeanzisha biashara hiyo anajua kipi sahihi kwake kufanya ili apate mafanikio.
Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara, labda kwa maisha kuwabana na kuona hawana namna bali kuanza biashara. Au wanaingia kwenye biashara kwa sababu wanaona wengine nao wapo kwenye biashara na kwa nje wanaonekana biashara zao zinaenda vizuri.
Sababu hizo siyo mbaya, ila mtu anapoingia kwenye biashara kwa sababu hizo, anapofika ndani anakutana na ukweli ambao unamuumiza zaidi. Aliyefikiri maisha ni magumu na hivyo akiingia kwenye biashara yatakuwa rahisi, anashangaa maisha ya biashara yanakuwa magumu zaidi kwake. Aliyeingia kwa sababu aliona wengine wanafanikiwa kwa nje, akifika ndani anaona biashara ni ngumu kuliko ilivyoonekana kwa nje.
Yapo maswali mawili muhimu sana kwa kila mtu kujiuliza kabla ya kuingia kwenye biashara yoyote ile. Kwa kujiuliza maswali haya, utaingia kwenye biashara ukiwa na uelewa sahihi, na ukijua ni hatua zipi sahihi kwako kuchukua ili kufanikiwa zaidi kwenye biashara unayofanya.
Swali la kwanza; Ni nani mwenye fedha zangu?
Nilishakuambia siku za nyuma kwamba hutafuti fedha bali unakusanya fedha. Fedha unayoitaka sasa, ipo kwenye mikono ya mtu mwingine. Hivyo hatua ya kwanza kabisa kwenye kufikiria biashara yako ni kujiuliza nani mwenye fedha zako.
Hapa unahitaji kuwajua wateja halisi wa biashara yako, watu ambao wana shida, wana changamoto, wana uhitaji ambao unaweza kuutimiza. Pia watu hao wana fedha ya kuweza kukulipa wewe kwa kile ambacho unawapa.
Kama hujawajua watu wenye fedha zako, ukianzisha biashara utakuwa unapoteza muda wako. Kwa sababu hata kama unaona wengine wanauza sana, utashangaa unakaa kwenye biashara na hupati mauzo makubwa kama wengine.
Kwa sababu unakua hujajua nani mwenye fedha zako na kumfuatilia huyo zaidi.
Kama uliingia kwenye biashara bila kujiuliza swali hili, kaa chini sasa hivi na jiulize nani mwenye fedha zako? Orodhesha sifa za watu ambao wanaweza kunufaika na aina ya biashara unayofanya, na wenye uwezo wa kulipia kile unachouza.
Ukishajua kwa hakika nani mwenye fedha zako, ni rahisi kumlenga huyo na ukaweza kumhudumia vizuri na wote mkanufaika sana.
SOMA; Sifa Tano (5) Za Biashara Inayoweza Kufikia Mafanikio Makubwa.
Swali la pili; jua ni kitu gani unabadilishana nao ili wakupe fedha hizo.
Baada ya kuwajua wenye fedha zako, unahitaji kujua kitu gani unahitaji kuwapa ili nao wakupe fedha walizonazo. Kwa sababu kila mtu amepata fedha yake ka uchungu, na hivyo hataki kuipoteza. Lazima uwe na sababu kubwa ya kumshawishi mtu akupe fedha zako. Kumbuka akishakupa fedha wewe, hawezi tena kuitumia kwa mambo yake mengine.
Hapa unahitaji kujua kwa hakika ni thamani gani unatoa kwa wateja wa biashara yako. Hapa unahitaji kujua kwa hakika ni mahitaji gani waliyonayo wateja wako ambayo unayatimiza, ni maumivu gani ambayo unayatuliza.
Kama huna sababu ya kutosha, ya kumshawishi mteja akupe fedha yake aliyoipata kwa shida, hutaweza kufanikiwa kwenye biashara yako.
Kwa sababu kumbuka mteja hanunui kwa sababu wewe unauza, wala hanunui kwa sababu anakuonea huruma. Bali mteja ananunua kwa sababu ana uhitaji, ana maumivu ndani yake ambayo hawezi kuendelea nayo na kuna mtu amemshawishi kwamba ana kitu cha kutimiza mahitaji yake au kutuliza maumivu yake.
Hivyo baada ya wewe kujua ni nani mwenye fedha zako, jua maumivu yake ni yapi, kisha mweleze jinsi kile unachouza kinavyoweza kutuliza maumivu aliyonayo.
Jiulize maswali hayo mawili muhimu kabla hujaingia kwenye biashara yoyote ile. Na kama uliingia kwenye biashara hujajiuliza maswali hayo, chukua muda ujiulize maswali hayo sasa ili upate majibu sahihi na utakayoyafanyia kazi. Pia endelea kujiuliza maswali hayo kila siku ili kuongeza wateja wapya na kuwapa watu sababu zaidi za kuendelea kununua kwako.
Kumbuka huhitaji kumuuzia kila mtu kwenye biashara yako, badala yake unahitaji kuchagua aina ya wateja ambao unaweza kuwafikia vizuri na ukawahudumia vizuri sana na hao watakuletea wateja wa aina hiyo.
Endesha biashara yenye mafanikio makubwa kwa kuchagua watu wenye uhitaji wa kile unachotoa kisha kuwahudumia vizuri sana.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha